29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MSANDO ATEULIWA KUHAKIKI MALI ZA CCM

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk. John Magufuli, ameunda tume ya chama hicho itakayokuwa na jukumu la kwenda kufuatilia mali za chama hicho nchi nzima.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa NEC (Itikadi na Uenezi), Humphrey Polepole ilitaja wajumbe walioteuliwa kuwa ni Dk. Bashiru Ali (Mwenyekiti) huku wajumbe wakiwa ni Walter Msigwa, Albert Msando, Galala Wabanhu (Hananasif) na Albert Chalamila.

Wengine ni William Sarakikya, Komanya Kitwara, Dk. Fenela Mukangara na Mariam Mungula.

Taarifa hiyo ya CCM ilieleza kuwa tume hiyo itafuatilia mali za chama hicho kokote ziliko na itamhoji kila mtu anayehusika katika chama na Serikali.

“Mtakwenda kumhoji mtu yeyote, viongozi na watendaji wa CCM katika mikoa, wilaya, kata, matawi na mashina mtoe ushirikiano ili kuhakikisha mali za CCM hazipotei…

“Nitoe wito kwa Watanzania wanaoshikilia mali za CCM wajitokeze na waseme ukweli kwa maslahi ya CCM,” alisema Rais Magufuli.

Awali akifungua kikao cha kwanza cha NEC baada ya kuamalizika kwa Mkutano Mkuu wa Tisa wa Taifa wa CCM, Rais Magufuli alisema yeye ni mtumishi wa CCM na siku zote atafanya kazi za chama na Serikali kwa kujitoa kwa bidii na umakini kwa kadri Mungu atakavyo mjalia.

Kikao cha NEC kimeelekeza viongozi, watendaji na wajumbe wa vikao vya uongozi ngazi ya mikoa, wilaya, majimbo, kata na matawi kuwa na utaratibu wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo kama ahadi mbalimbali na Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyoelekeza.

Akitoa maelekezo mahususi na ya jumla Rais Magufuli, aliwataka wajumbe wa NEC kutambua wajibu mkubwa walio nao wa kusimamia chama na Serikali.

“Tumekuwa viongozi kwasababu Mungu amependa, tukafanye kazi, tukatende haki, tusiwaonee watu, tukatimize wajibu wetu, tukasimamie maadili ya chama,” alisema

Akizungumza katika kikao hicho Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), Dk. Ali Mohamed Shein, amempongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri ya kutetea wanyonge na kulinda rasilimali za wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles