30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MSAJILI HAZINA ANG’OLEWA

Lawrence Mafuru
Lawrence Mafuru

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli amemng’oa Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru na nafasi yake kurithiwa na Dk. Osward Mashindano.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu jana usiku, ilieleza kuwa Dk. Mashindano anachukua nafasi hiyo na Mafuru atapangiwa kazi nyingine.

Mafuru, hivi karibuni aliibuka na kauli tata ambayo ilionekana kupingana na Rais Magufuli kuhusu uamuzi wa baadhi ya taasisi za umma kuweka fedha katika Fixed Deposit Accounts (akaunti maalumu).

Kauli hiyo aliitoa Novemba 30, mwaka huu katika mahojiano maalumu na redio moja nchini. Alisema haiwezekani kwa watumishi wa umma kuiba fedha zinazowekwa katika Fixed Deposit Accounts kwa sababu miamala ya benki ni ya uwazi.

Alisema hizo ni tuhuma tu na Serikali imemwagiza CAG kuchunguza.

“Nimefanya kazi katika taasisi za benki kwa miaka 20, sijawahi kuona watumishi wa umma wakichota hela kwenye fixed deposit account.

“Pale kwenye benki kuna miamala ya aina mbili tu, ya kuweka na kutoa. Usipoweka wazi wakati wa kuweka, siku utakapozitoa itaonyesha tu,”  alisema Mafuru.

Alisema hakuna kosa kwa taasisi za Serikali kuweka fedha katika akaunti hizo, lakini Serikali sasa imeamua kuzihamishia Benki Kuu (BoT) ili iwe rahisi kuzifuatilia.

Kauli hiyo ya Mafuru ilitanguliwa na ile ya Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, ambaye alisema si kosa kisheria kwa taasisi kufungua akaunti maalumu katika benki ya biashara.

Novemba 26, mwaka huu, Rais Magufuli alifichua siri ya hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Alisema alilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya bodi hiyo kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kuwekwa katika akaunti maalumu (Fixed Account) katika benki kadhaa za biashara.

Bodi hiyo ilitoa idhini ya kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati kuna agizo la Rais la kupiga marufuku taasisi za umma, mashirika ya umma, idara za Serikali, wakala na wizara kuweka fedha zao katika benki za kibiashara.

Fedha hizo zinatakiwa zifunguliwe akaunti BoT.

Hatua hiyo ilitokana na uamuzi wake wa kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, na saa chache akateua Naibu Kamishna Mkuu mpya.

Ikulu bila kueleza sababu, ilisema kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja bodi nzima.

Aidha, pamoja na kuivunja bodi hiyo, alimteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada ya Dk. Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Lusekelo Mwaseba.

Akihutubia katika mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Makao Makuu ya chuo hicho, Bungo wilayani Kibaha mkoani Pwani, Dk. Magufuli alisema aliitumbua bodi hiyo kutokana na kukiuka taratibu.

Alieleza kuwa kitendo chao cha kuidhinisha fedha hizo kuwekwa katika benki tofauti, ni tofauti na maelekezo kwani huo ndio ulikuwa mchezo unaofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali.

Rais Magufuli alisema kumekuwa na mchezo wa wakuu wa taasisi mbalimbali kuchukua fedha na kuziwekwa kwenye akaunti maalumu ambako serikali inakwenda kukopa kwa gharama kubwa.

 MABADILIKO

Rais Magufuli pia amefanya uteuzi wa katibu mkuu mmoja na mkuu wa mkoa mmoja na mabadiliko madogo katika wizara na mikoa.

Amemteua Profesa Faustin Kamuzora kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Katibu Mkuu Mawasiliano.

Rais Magufuli amemteua pia aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhandisi Mathew Mtigumwe kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo anayeshughulikia Kilimo akichukua nafasi ya Dk. Frolence Turuka aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Dk. Turuka anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Job Masima ambaye ameteuliwa kuwa balozi.

Rais Magufuli amemteua Dk. Maria Sasabo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na atakuwa akishughulikia mawasiliano, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Profesa Kamuzora ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais.

“Pia Rais Magufuli amemteua Mhandisi Angelina Madete kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Maria Sasabo aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

“Aidha, Rais Magufuli amemteua Dk. Aloyce Nzuki kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,” ilieleza taarifa hiyo.

 SENDEKA AONDOLEWA CCM

Mbali na uteuzi huo Rais Magufuli, amemteua Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe.

Sendeka anachukua nafasi ya Dk. Rehema Nchimbi ambaye amehamishwa kituo cha kazi na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles