THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Azam, Aristica Cioaba, ameendelea kukiweka fiti kikosi chake kuhakikisha kinakuwa na moto wa kuotea mbali katika mechi zao za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Azam waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Biashara United katika mchezo wao wa mwisho wa ligi hiyo kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Ushindi huo walipata wakiwa wametoka kupoteza mechi mbili mfululizo, wakifungwa bao 1-0 na Simba pamoja na Ruvu Shooting.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Jafar Iddy, alisema baada ya kumaliza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Biashara United, benchi la ufundi liliongeza zaidi mazoezi katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama kupisha mechi za kimataifa.
“Wachezaji wanaendelea na mazoezi ikiwa ni maandalizi ya mechi ambazo zinatukabili mbele yetu, ligi imesimama hivyo huu utakuwa muda mzuri kwa sisi kujiandaa vizuri kwa ajili ya michezo inayotukabili,” alisema.
Alisema Cioaba anautumia muda huu kuhakikisha wachezaji ambao hawajaenda kwenye timu zao za Taifa, wanakuwa fiti na kuyafanyia kazi baadhi ya makosa.
Idd alisema kwa sasa wanaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Azam Complex na kwamba hawana mchezaji ambaye ni majeruhi.