25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa maji Songwe mbioni kuanza

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

KATIBU Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema Serikali inatarajia kuanza mradi mkubwa wa maji utakaohudumia miji mbalimbali katika Mkoa wa Songwe ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama.

Aliyasema hayo hivi karibuni alipotembelea eneo la Mto Bupigu, Kijiji cha Bupigu wilayani Ileje Mkoa wa Songwe kwa dhamira ya kukagua vyanzo toshelevu vya maji katika miji yenye changamoto ya huduma ya maji.

Wataalamu wa sekta ya maji wakiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (Wapili kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga, wakati wa kukagua vyanzo vya maji katika miji yenye changamoto za huduma za maji.

“Kuna chanzo tunachokitarajia kuchukua maji takriban kilomita 75 kutoka Bupigu kuelekea mji wa Tunduma. Ni mradi ambao tunautengeneza ili tutafute fedha za kuanza kuujenga,” amesema Mhandisi Sanga.

Amesema Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa maeneo ya mijini mkoani humo na kwamba jitihada za makusudi zinaendelea kuchukuliwa ili kuwa na huduma toshelevu ya maji kwa wakazi wa miji hiyo.

“Kwa Mkoa wa Songwe, tunatambua changamoto kubwa ya maji ipo katika maeneo ya mijini, maeneo ya vijijini Serikali kupitia RUWASA imefanya kazi kubwa lakini mijini mathalan katika mji wa Tunduma mahitaji ni takriban lita milioni 17 kwa siku wakati maji yanayozalishwa ni chini ya lita milioni tano kwa siku,” amesema.

Amesema Serikali imelenga kutoa maji Mto Bupigu na kuyafikisha katika mji wa Ileje ambapo ndipo chanzo kilipo, vijijini 14 vipate maji kupitia mradi huo, makao makuu ya Mkoa wa Songwe yaani Vwawa, mji wa Tunduma, Mlowo na Mbozi.

Amefafanua kwamba matarajio ya Serikali ni kuhakikisha vyanzo toshelevu vya maji vinatumika kwa kuwa na miradi mikubwa ya maji ili kuwaondolea adha wananchi.

“Tunatarajia kutumia Mto Bupigu kujenga mradi mkubwa ambao utaondoa kabisa tatizo la maji katika mji wa Tunduma; ni ahadi ambayo tulikwishaitoa kupitia viongozi mbalimbali wa kitaifa ambao walifika huku,” amesema.

Amesema kufika kwake hapo ni kuashiria kwamba mradi huo sasa upo katika hatua za kutengenezwa ili uweze kuanza na kuwaondolea wakazi wa Tunduma na miji mengine mkoani humo changamoto ya upatikanaji wa maji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles