22.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Posta watanua wigo usafirishaji sampuli za maabara

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC) limeingia makubaliano na Kampuni ya Tutume kusafirisha sampuli za kibaiolojia ili kurahisisha utoaji huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Postamasta Mkuu, Macrice Mbodo, amesema wamepewa jukumu na Serikali kusafirisha sampuli za maabara kutoka vituo vya afya kwenda maabara za uchunguzi na kurejesha majibu baada ya uchunguzi.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya usafirishaji sampuli za kibaiolojia kati ya Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya Tutume.

Amesema sampuli zinazosafirishwa ni za magonjwa ya kawaida kama vile Kifua Kikuu, HIV na zinazotokana na magonjwa ya mlipuko kama Uviko – 19.

“Usafirishaji wa sampuli za maabara unahusisha kutoka vituo vya afya ngazi ya kwanza vinavyotumika kukusanya sampuli kutoka kwa wananchi kwenda katika vituo vya afaya ngazi ya pili vinavyotumika kuhifadhi na kuchakata sampuli.

“Sehemu ya pili inahusisha kutoka kwenye vituo vya afya ngazi ya pili kwenda kwenye maabara za uchunguzi kisha majibu yanarudishwa kwa mfumo huo,” amesema Mbodo.

Amesema kampuni hiyo itasafirisha sampuli za maabara na majibu yake kutoka vituo vya afya ngazi ya kwanza kwenda ngazi ya pili nchi nzima na kwamba shirika litasafirisha sampuli kutoka vituo ngazi ya pili kwenda maabara za uchunguzi.

Amesema pia wameajiri kwa njia ya uwakala vijana waendesha bodaboda zaidi ya 450 nchi nzima na kupitia ushirikiano huo wataajiri zaidi.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema ushirikiano huo utaiwezesha Serikali kufikia malengo yake na kuimarisha huduma za afya hasa vijijini na kuitaka kampuni hiyo kuwa mfano mzuri kwa mafanikio ya shirika la posta.

Amewaomba wasafirishaji wote wa bidhaa na huduma mbalimbali nchini kutumia mfumo wa anwani za makazi ili kutatua matatizo ya wananchi.

“Weledi na uaminifu utawale katika kazi mnazozifanya, ushirikiano wenu ukatoe matunda ya kuboresha huduma.

“Ushirikiano huu ni wa manufaa kwa pande zote mbili hasa kwa wananchi, utaongeza wigo wa utoaji huduma kwa jamii, utaongeza tija na hatimaye mapato ndani ya shirika na serikali kwa ujumla,” amesema Nape.

Amesema shirika hilo lina uzoefu mkubwa katika nyanja ya usafirishaji na kwamba lina vifaa vya kisasa vya kutosha yakiwemo magari na pikipiki kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

Amelitaka Shirika la Posta kutumia fursa ya uwekezaji katika sekta ya kilimo kwa kusafirisha mbegu na pembejeo mbalimbali.

Kwa upande wae Mkurugenzi wa Kampuni ya Tutume, Misana Manyama, amesema wana uzoefu wa kutosha wa kusafirisha sampuli za kibaiolojia na kuahidi kuitumia vyema fursa hiyo kwa kufanya kazi kwa weledi.

Amesema pia wameajiri vijana wa bodaboda 1,400 na kupitia ushirikiano huo wataongeza ajira zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles