27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MRADI WA MAJI KUGHARIMU BILIONI 375.4/-

Na SAMWEL MWANGA -SIMIYU

TANZANIA kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani, Mfuko wa Mabadiliko ya Tabianchi (CGF) na wananchi watatumia Sh bilioni 375.4 kutekeleza mradi wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi mkoani Simiyu.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe, alipofungua kikao cha wadau wa mabadiliko ya tabianchi kilichofanyika Bariadi, Simiyu.

Alisema moja ya shughuli muhimu na kubwa katika utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi ni ufikishaji wa huduma ya maji ya Ziwa Victoria katika mji wa Bariadi ambao ni makao makuu ya Simiyu na wilaya za Bariadi, Busega na Itilima kwa awamu ya kwanza na baadaye katika wilaya ya Meatu na Maswa.

Alisema upatikanaji wa maji Simiyu uko chini ikilinganishwa na wastani wa kitaifa na kwa kutambua hali hii hivyo Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilibuni mradi huu ili kupata suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwa wananchi na mifugo ambayo ni moja ya shughuli za kiuchumi za wananchi wa mkoa huu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, ameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo utakaowasaidia wananchi na utakuwa chachu katika ujenzi wa viwanda mkoani humo kwa kuwezesha upatikanaji wa maji ya uhakika.

“Wananchi wote wa Simiyu wanausubiri sana mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria, pia mkoa wetu unaenda katika uwekezaji wa viwanda vikubwa na changamoto tuliyonayo ni suala la upatikanaji wa maji ya uhakika, utekelezaji wa mradi huu utatusaidia katika viwanda,” alisema.

Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo, alisema Simiyu ni miongoni mwa mikoa yenye kiwango cha chini cha upatikanaji wa huduma ya maji ambayo Serikali imetoa kipaumbele cha kuipa fedha kutoka katika mfuko wa maji ili kutekeleza miradi ya maji itakayoibuliwa na kuwasilisha maandiko yake wizarani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles