30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MADIWANI CHADEMA WADAI CCM IMEWASHAWISHI KUHAMA

Na ABRAHAM GWANDU-ARUSHA

BAADA ya Kaimu Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Simanjiro, Meshak Tureto, kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), madiwani wa chama hicho wameibuka na kudai kuwa, pamoja na kushawishiwa kuhama, lakini hawatatetereka, bali wataendelea kuwatumikia wananchi hadi watakapomaliza kipindi cha miaka mitano.

Tureto alihamia CCM hivi karibuni kwa sababu ya kile alichokaririwa akisema kuwa, ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Dk. John Magufuli ya kuwaletea maendeleo wananchi tangu ilipoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Katibu wa Madiwani wa Chadema wilayani, Filimon Eyogo, alisema tetesi za madiwani wa chama hicho kuhamia CCM ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ni za uwongo na wataendelea kushirikiana na Serikali wakiwa bado viongozi wa Chadema.

Alisema mara zote watu wanaohama vyama husema maneno ya uongo na uzushi kama njia ya kujiongezea thamani huko wanakotaka kujiunga ili waaminike na kukubalika.

Aliwatoa wasiwasi wapiga kura wao juu ya uvumi unaoenezwa na watu aliodai ni washindani wao kisiasa kuwa madiwani wanane wa Chadema wilayani Simanjiro nao watajiunga na CCM wakati wowote.

“Chadema Simanjiro bado iko imara, hizi sababu zinatotajwa wakati wanaondoka hazina mashiko, mbona sisi ambao ni wawakilishi wa wananchi tunaziona changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo yote yawe ya CCM au Chadema bado zipo nyingi? Wenzetu wanaoondoka watuambie vizuri hayo maendeleo ni yao binafsi au ya wananchi.

“Sijui wamevutiwa na nini, wakishaondoka kila mmoja anakuja na hoja ya utendaji kazi wa Serikali, kwani huwezi kuunga mkono ukiwa kiongozi, kama hutaweza ukiwa madarakani hutaweza ukiwa raia, nadhani hizi hoja ni dhaifu. Tulichaguliwa na wananchi, hakuna atakayeondoka hadi Uchaguzi wa 2020,” alisema Eyogo.

Naye Diwani wa Naberera, Yamat Hhayo, alisema hakuna sababu ya wananchi wa Simanjiro kupata hofu ya viongozi wao kuhama, bali wataendelea kutimiza ahadi walizotoa wakati wakiomba kura.

“Tunapoendelea kuwatumikia wananchi wetu ndio tunamuunga mkono Rais Magufuli, huwezi kuacha kuwatumikia wananchi halafu ukasema unamsaidia wakati wewe si kiongozi mahala popote,” alisema Yamat.

Kwa upande wake, Diwani wa Lobosoriet, Ezekiel Olosenga, alisema viongozi wote wa vyama vya upinzani wanaohama na kujiunga na CCM ni walafi na wanafuata ulaji na si kuunga mkono kazi kama wanavyoaminisha wananchi.

“Sisi wote kila mmoja kwa wakati wake kwa muda sasa tunakutana na vishawishi vya fedha na madaraka kutoka kwa watu ambao kwa sasa hatutawataja, lakini tunakataa kwa sababu lengo la kuomba kura wananchi si kujipatia fedha, bali ni kuwatumikia kwa uaminifu na kusaidiana nao kuleta maendeleo,” alisema Olosenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles