25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mradi wa kudhibiti wizi wa mapato wazinduliwa Kaliua

Na Allan Vicent, Kaliua

HALMASHAURI ya wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora imezindua mradi wa Teknolojia ya ‘CCTV Camera’ uliofungwa katika Kituo Kikuu cha mabasi kwa lengo la kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza makusanyo ya halmashauri.

Mradi huo umezinduliwa jana na Kiongozi wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Lt. Josephine Paul Mwambashi ambapo ameipongeza halmashauri hiyo kwa kubuni mradi wenye tija kubwa katika suala zima la udhibiti wa mapato.

Alisema mradi huo umetekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mbio hizo kwa mwaka huu inayosema TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) ni msingi wa Taifa endelevu, itumie kwa usahihi na uwajibikaji.

Alishauri stendi hiyo kuboreshwa ili kuongeza ubora wake na kuvutia watumiaji ambao ni madereva wa vyombo vya usafiri hususani mabasi yanayopita hapo kwenda mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Tabora.

Awali akisoma taarifa ya mradi huo Ofisa TEHAMA wa halmashauri hiyo Aggrey Lubango alisema kuwa mradi huo ulioanza kutekelezwa Machi 8, mwaka huu utasaidia sana kudhibiti mianya yote ya upotevu wa mapato.

Aidha alisema kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatarahisisha kwa kiasi kikubwa utunzaji kumbukumbu za mapato na kuongeza uwazi katika suala zima la ukusanyaji mapato na hivyo kuongeza mapato ya ndani.

Lubango alibainisha kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha sh mil 6.7 ikiwa ni gharama za manunuzi ya vifaa vya mfumo huo wa CCTV Camera na kulipa wataalamu waliozifunga.

Aliongeza kuwa kabla ya kuanza mradi huo mabasi yaliyokuwa yanaingia katika stendi hiyo na kulipiwa kwa wastani yalikuwa 45 tu kwa siku lakini baada ya kufungwa mfumo huo idadi ya mabasi yanayoingia na kulipiwa ushuru sasa yamefikia 60 kwa siku.

Aidha alisema camera za mfumo huo zimefungwa katika mageti yaliyoko mpakani katika kata ya Kashishi (mpaka wa wilaya ya Kaliua na Kahama) na kata ya Usindi iliyoko mpakani mwa wilaya ya Urambo na Kaliua ili kuhakikisha mazao yote yanayosafirishwa nje ya wilaya hiyo yanalipiwa ushuru.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles