Na Allan Vicent, Tabora
MRADI wa kuimarisha huduma za afya nchini wa HPSS (Health Promotion and System Strengthening Project) uliokuwa ukitekelezwa katika Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa na Tabora umehitimishwa kwa mafanikio makubwa katika mikoa hiyo.
Mradi huo wa kimkakati wa miaka miwili uliotekelezwa na serikali ya Tanzania kwa ushirikano na serikali ya Uswisi tangu Novemba 2019 hadi Oktoba 2021 umewajengea uwezo mkubwa wataalamu wa afya na kuanza kutoa huduma bora kwa jamii.
Akizungumza katika mkutano wa hitimisho ya mradi huo jana Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora anayeshughulikia Rasilimali watu Hamis Mkunga alisema mradi umeboresha utoaji huduma za afya kwa kiasi kikubwa katika afua mbalimbali.
Alitaja baadhi ya mambo yaliyofanywa na mradi wa HPSS Tuimarishe afya katika kipindi hicho kuwa ni kuzijengea uwezo timu za uratibu wa huduma za Bima ya Afya iliyoboreshwa jambo ambalo limepelekea kuongeza idadi ya wanachama wa mfuko huo.
Manufaa mengine ni kuimarisha mfumo wa taarifa za Bima ya afya iliyoboreshwa, kuwajengea uwezo Maafisa Afya, Wataalamu wa Vifaa Tiba na Timu za Afya za Mikoa hiyo (RHMT).
Mkunga aliwataka Makatibu Tawala wa Mikoa hiyo, Waganga Wakuu (RMO’s) na Wataalamu wa Afya kusimamia na kuendeleza yale yote yaliyofanywa na mradi huo.
Mtaalamu Mshauri wa Mradi huo Emanuel Mwanga alisema kuwa kupitia mradi huo huduma mbalimbali za afya zimeboreshwa katika Mikoa hiyo ikiwemo kuziongezea weledi timu za afya, kuboreshaa vifaa tiba na mifumo ya uratibu wa CHF iliyoboreshwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dk.t Simon Chacha alipongeza mradi huo kwa kuwasaidia kupata mafunzo, vitendea kazi na kuongeza mapato kwa kusajili wanufaika wengi zaidi wa CHF iliyoboreshwa.Â
Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Geofrey Maleale alishauri Uongozi wa Mikoa hiyo kushughulikia changamoto za afya zilizopo katika maeneo yao ambazo hazikumalizwa na mradi huo.