26.7 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa AGRI-CONNECT wanufaisha wakulima Mbeya

Na Mwandish Wetu, Mtanzania Digital

Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) unaendelea na utekelezaji wa mradi wa Agri-Connect unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) katika Mkoa wa Mbeya wenye lengo la kuboresha miundombinu ya barabara zinazounganisha maeneo ya uzalishaji, utunzaji, uchakataji na masoko katika maeneo yanayolimwa mazao ya biashara ili kongeza tija katika sekta ya Kilimo na kukuza uchumi.

Hayo yameelezwa na Meneja wa TARURA Wilaya ya Mbeya, Mhandisi Selemani Mziray alipokuwa katika ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabara ya Inyala–Simambwe yenye urefu wa Km 16.7 na ujenzi wa barabara ya Lupeta –Wimba–Izumbwe yenye urefu wa Km 10.1 zote kwa kiwango cha lami zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Mhandisi Mziray alisema zaidi ya Sh bilioni 11 zilitengwa katika ujenzi wa barabara hizo na tayari Km 16.7 za ujenzi wa Barabara ya Inyala–Simambwe zimekamilika na mradi wa ujenzi wa Lupeta–Wimba–Izumbwe umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari 2024.

“Zaidi ya bilioni 11 zilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii wilayani Mbeya ili kuwawezesha wakulima katika shughuli zao za usafirishaji wa mazao kutokana na maeneo hayo kujihusisha na kilimo cha biashara kama vile chai, kahawa,” alisema Mhandisi Mziray.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Inyala, Fidelis Mabena ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa barabara ya Inyala–Simambwe kwani imekuwa mkombozi mkubwa hasa katika usafirishaji wa mazao yao tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa changamoto kuleta mazao kutoka vijijini hadi sokoni na kuongeza kuwa barabara hiyo pia imetoa fursa kwa vijana wa bodaboda kufanya shughuli zao kwa urahisi.

“Kabla ya ujenzi wa barabara hii ilikuwa ni changamoto kwa wakazi wa Inyala katika usafirishaji wa mazao ila baada ya kukamilika kwa barabara hii sasa tunasafirisha mazao yetu kwa urahisi kutoka shambani kwenda kwenye masoko, barabara hii imetunyanyua sana wana Inyala hatuna budi kuishukuru Serikali,’’ alisema Fidelis.

Faines Mwanchole, Mkazi wa Kijiji cha Wimba alisema zamani wakati wa kujifungua kwakina mama walikuwa wanapata shida kufika hospitali kwa sababu ya ukosefu wa barabara.

Mradi wa Agri-Connect unaendelea kutekelezwa katika Mkoa wa Mbeya katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ili kuondoa vikwazo kwa wakulima katika usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani kwenda kwenye masoko pamoja na kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles