Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MR Tanzania 2015, Muhammad Khalil (32) na David Mwakalebela (56), wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka saba ikiwemo kuishi nchini bila kibali na kumsaidia kutoa taarifa za uongo.
Mshtakiwa Muhammad maarufu kwa jina la Nauman Khalil Muhammad na Mwakalebela, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Respicius Mwijage.
Akiwasomea mashtaka Mwendesha Mashtaka wa Uhamiaji, Method Kagoma, alidai mshtakiwa Muhammad anakabiliwa na mashtaka sita.
Alidai Januari 29 mwaka huu katika ofisi za uhamiaji akiwa raia wa Pakistan alikutwa akiishi nchini kinyume cha sheria.
Mshtakiwa huyo anadaiwa Oktoba 10 mwaka jana, katika ofisi za uhamiaji alitoa taarifa za uongo katika fomu zake za kuomba hati ya kusafiria namba 946316 kwa lengo la kupata hati hiyo.
Shtaka la tatu anadaiwa katika tarehe hiyo, aliwasilisha cheti cha kuzaliwa cha kughushi namba 002538000.
Katika shtaka la nne anadaiwa alitoa maelezo ya uongo kwa kuwasilisha kitambulisho cha uraia kilichosajiliwa kwa jina la Amina Alli Muhammad Noor Muhammad, akimtambulisha kwamba ni mama yake kwa lengo la kupata hati ya kusafiria.
Shtaka la tano anadaiwa kuwasilisha nakala ya hati ya kusafiria namba AB228350 ya mama yake, ili kupata hati hiyo ya kusafiria.
Katika shtaka la sita inadaiwa Januari 29 mwaka huu, alitoa maelezo ya uongo kwa kusaini na kuweka alama ya vidole katika fomu ya kusafiria namba 097/1752.
Shtaka la saba anadaiwa kuwa Oktoba 20, 2015 katika ofisi za Idara ya Uhamiaji jijini Dar es Salaam, Mwakalebela akiwa kama Mtanzania alimsaidia mshtakiwa wa pili Mohammad kuwasilisha hati za kughushi kwa ajili ya kujipatia hati ya kusafiria.
Hata hivyo, Mwakalebela alikana mashtaka hayo wakati mshtakiwa wa pili alikiri kufanya hivyo.
Hakimu Mwijage aliwataka washtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni 2 na kesi hiyo itatajwa Februari 17. mwaka huu.