CHRISTOPHER MSEKENA
MIONGONI mwa video zinazofanya poa kwa sasa kwenye mtandao wa YouTube ni ile ya wimbo, Mpaka Kesho kutoka kwenye albamu, Afro East ya Harmonize.
Video hiyo ambayo imefanyika kwenye mandhari nzuri huko Manyara nchini Tanzania, imebeba kisa cha kijana mmoja mwenye asili ya kizungu (Mr Simon) aliyemuoa kinguvu mpenzi wa Harmonize ambaye ni Mimi Mars.
Swaggaz tumefanya mahojiano na Mr Simon, raia wa Norway anayeishi jijini Arusha akifanya shughuli za kusaidia jamii pamoja na sanaa ya muziki kama prodyuza na msanii akiwa ameshatoa wimbo wake, Yes I Do.
SWAGGAZ: Simon ni nani na ilikuwaje ukaingia kwenye sanaa ya muziki?
Mr Simon: Nilizaliwa kwenye familia ya kikristo ya kanisa la Pentekoste katika Mji mdogo wa Drammen huko Norway na hapo ndio safari yangu ya muziki ilipoanzia.
Nilianza kujifunza kupiga ngoma na vyombo kadhaa ya muziki pamoja na kuimba kwenye bendi ya kanisa.
Pia nilikwenda shule na nilipomaliza nikaanzisha kampuni yangu nikiwa na miaka 19 na ilifanikiwa sana na baadaye nikaamua kurudi kwenye kitu ninachokipenda yaani muziki na kuanzia miezi miwili ijayo basi nitaingia rasmi kwenye muziki kwa ukamilifu.
SWAGGAZ: Sababu gani zilifanya utoke Norway uje Tanzania kufanya shughuli zako?
Mr Simon: Wakati nafikiria kufanya ninachokipenda na sio kufanya kazi tu ili kupata fedha, nilianza kusafiri sehemu mbalimbali ulimwenguni kurudisha na kusaidia wengine.
Nilikuja Arusha kama mtu wa kujitolea miaka 2 au 5 hivi iliyopita na tangu wakati huo niliipenda Tanzania, muziki na maisha ya watu wake.
Ngoma ya kwanza kuisikia ni Kwagwaru ya Harmonize na Diamond Platnumz, Mhudumu ya Aslay na wamekuwa wasanii wangu pendwa na kiukweli napenda Afro-pop na Bongo Fleva.
Nilianza kutoa misaada nchini Norway baadaye nikaja hapa Arusha, kwa hivyo nimekuwa na miradi michache hapa tangu nije na moyo wangu upo zaidi Tanzania kwahiyo kwa miaka miwili iliyopita nimekuwa na kwenda Norway na kurudi Tanzania.
Na nimekuwa nikifanya kazi zangu za uzalisha muziki na kuimba kimya kimya ila nadhani sasa umefika muda wa kuonyesha kazi zangu ulimwenguni.
SWAGGAZ: Ulikutana vipi na Harmonize na mkafanya kazi pamoja?
Mr Simon: Ni stori ya kuchekesha ila nilikwenda kwenye mahojiano ya Radio 5 Arusha na mtangazaji Dj Hazuu akanikutanisha na Hanscana ambapo alimuuliza Hazuu kama naweza kutokea kwenye video ya Mpaka Kesho.
Walitupa hiyo taarifa usiku kwa hiyo ikabidi tuzunguke Arusha nzima kutafuta suti na saa 12 asubuhi tukaendesha gari mpaka Karatu kwenda kufanya video.
SWAGGAZ: Harmonize na timu yake ya Konde Gang ni watu wa aina gani?
Mr Simon: Nina mapenzi mengi tu ya kwa Harmonize na timu yake. Timu yake yote ilinitunza vyema, walithamini bidii yangu na sote tulikuwa na wakati mzuri wakati tunashuti video.
Naendelea kuwasiliana nao hadi sasa na tumekuwa marafiki, ni wanyenyekevu na shauku kubwa kwenye muziki wake.
SWAGGAZ: Changamoto gani ulikutana nazo ulipokuwa unafanya video na Harmonize?
Mr Simon: Changamoto kubwa ni ile ya kutafuta suti usiku na kuendesha umbali mrefu bila kulala kwenda kufanya video pamoja na tayari la gari letu kupasuka.
Nyingine ni ndogo ndogo tu labla na pale ambapo ilitakiwa nionyeshe nina hasira kwa Mimi Mars. Unajua haikuwa rahisi kukasirika kwake (anacheka) ni msichana mzuri na mimi sio mwigizaji bora ila tulifanya.
SWAGGAZ: Kwa muda mfupi ambao video imetoka, kuna faida yoyote umepata?
Mr Simon: Nimekuwa nikifanyiwa mahojiano mengi kwenye redio na hivi kwenye gazeti na faida zingine nadhani nitazipa hapo mbeleni kwa sababu ndio kwanza video imetoka.
SWAGGAZ: Baada ya kufanya video ya Harmonize, kuna mipango yoyote?
Mr Simon: Nina mipango mingi mbeleni, hivi karibuni nimeachia wimbo wangu Yes I Do, namshukuru Dj Hazuu kwa kunipa mtandao mkubwa wa wasanii wakubwa hapa Tanzania.
Kwahiyo naomba sapoti kwa mashabiki, wanaweza kunifollow kwenye Instagram, Facebook, YouTube, Audiomack na soundclouds natumia @mrsimonofficial, nawashukuru watu wote wanaonipa sapoti, naheshimu mchango wao.
Pia wasanii ambao nimeshirikisha kwenye ngoma yangu, Yes I Do, Jimmy Jay, 25Ren na prodyuza wangu msaidizi GD Beats.