MSANII wa nyimbo za asili, Mrisho Mpoto, ameweka wazi kwamba wasanii wa sasa wengi wao wanaangalia biashara zaidi kuliko kujituma kama walivyokuwa wakifanya wasanii wa zamani.
Mpoto aliweka wazi hayo jana wakati alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba, Rai na The African.
“Mfano mzuri Banana Zoro na Q Chief, ni watu wenye sauti zenye mvuto wakiimba lazima uwakubali, lakini kwa sasa staili yao imebadilika tofauti na awali, wanachoimba kinalenga masilahi tofauti na walipotoka,” alieleza.
Mpoto aliongeza kwamba, kama wasanii hao watarudi kwenye staili zao za zamani watakubalika zaidi kwa kuwa wana mashabiki wengi na wataongeza wengine ambao wanaonekana kuwaacha kutokana na kubadilisha aina ya muziki wao.