YOHANA PAUL – MWANZA.
MAPEMA mwezi huu, uongozi wa Chuo Cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ulifanya ziara mkoani Mwanza huku malengo makuu yakiwa ni kutembelea na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria, inayolenga kutatua changamoto ya usafiri kwa maeneo yanayozunguka ziwa hilo.
Miongoni mwa miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Chelezo, meli mpya na ukarabati wa meli katika eneo la Mwanza Kusini, ambapo baada ya kujionea miradi hiyo viongozi waliweka wazi kuridhishwa na maendeleo ya miradi japo walionyeshwa kutofurahishwa kuona kazi zikiratibiwa na kusimamiwa kwa kiwango kikubwa na wahandisi wageni kutoka nchini Korea.
Akizungumuzia hali hiyo Mkuu wa NIT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Profesa Zacharia Mganilwa, alisema ili kukabiliana na upungufu wa wataalamu wazawa waliojionea katika sekta ya uhandisi wa meli, wameamua kuja na mtaala mpya ili waanze kuzalisha wahitimu wenye taaluma ya usanifu na ujenzi wa meli.
Profesa Mganilwa alisema tayari wameshapanga kuanza kutoa mafunzo ngazi ya Stashahada ya ujenzi wa meli sambamba na Shahada ya kwanza ya Usanifu wa Meli ambapo kwa mwaka wa masomo 2020/2021 wanategemea kusaili wanafunzi 50 wa stashahada ya ujenzi wa meli na wanafunzi 30 wa usanifu wa meli.
Kwa ujumla, mipango ya NIT kuja na mtaala wa wahandisi wa meli unaunga mkono sera za serikali ya awamu ya tano ambayo mara kadhaa imekuwa ikisisitiza kupunguza utegemezi wa wahandisi wa kigeni na badala yake kutoa kipaumbele kwa wahandisi wazawa na kuhamasisha kazi za za ujenzi zilizo ndani ya uwezo wao kuratibiwa na kusimamiwa na kampuni za wazawa.
Uanzishwaji wa mtaala huo utasaidia kupanua wigo wa soko la ajira nchini kwani inawezekana kabisa baadhi ya wahandisi wenye taaluma zingine watatumia fursa hiyo kusoma mafunzo hayo ili kuwawezesha kupata ajira katika nyanja hiyo.
Kama NIT watatekeleza na kusimamia vilivyo ujio wa mtaala huo mpya, watasaidia kuongeza waajiriwa wenye taaluma husika katika MSCL iliyopewa mamlaka ya kusimamia huduma za meli nchini na pengine kuongeza weredi na ufanisi wa kampuni hiyo kwa kutumia taaluma yao.