24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MPAKISTAN ANAYEDAI KUWA NA NGUVU ZAIDI DUNIANI

Khan-Baba-Pakistan-Hulk3-600x823

TANGU vikatuni vya Hulk, jitu la kutisha na lenye nguvu ijapokuwa la kufikirika vilipoanzishwa mapema katika miaka ya 1960, mashabiki wamekuwa wakishangazwa na ushupavu au nguvu zaidi kuliko ghadhabu zake.

Tangu hapo kikatuni hiki kikapata nafasi katika tasnia ya filamu, ambako alizidi kujipatia umaarufu miongoni mwa mashabiki kwa namna alivyo.

Kuanzia hapo wale binadamu halisi wenye nguvu na maumbo makubwa wakajipatia au kujipachika u-Hulk hususani nchini Marekani.

Katika Bara la Asia kulikuwa na Hulk wa Iran na sasa amejitokeza Hulk wa Pakistan, ambaye ndiye makusudio ya makala haya.

Akiwa na uzito wa kilo 436, Arbab Khizer Hayat ameonesha matendo mengi kama vile kusimamisha trekta kwa mikono mitupu.

Pia ana kundi kubwa la wafuasi katika mji wake wa nyumbani wa Mardan, Pakistan.

Arbab Khizer Hayat, maarufu kama Hulk wa Pakistan mwenye umri wa miaka 25 na urefu wa futi 6 na inchi 3 ana ndoto za kuiwakilisha Pakistani katika mchezo wa mieleka wa uzito wa juu unaotambuliwa na Chama cha Mchezo wa Mieleka Duniani (WWE).

Hayat ni mtu mwenye mwili mkubwa, anayehaha kuhakikisha analinda umbo lake hilo la kutisha.

Mieleka na unyanyuzi wa vitu vizito ni mchezo unaopendwa na wengi.

Hata hivyo, linapokuja suala la mtu kudai kuwa na nguvu kuliko wote Pakistan huku akijiaminisha kuwa ni mwenye nguvu dunia bila kuthibitisha hilo, kunashangaza wengi.

Hayat alianza kunenepa katika umri mdogo na akavutiwa na mchezo wa mieleka na kunyanyua vitu vizito na hivyo kujiwa na ndoto ya kuwa mtu mwenye nguvu duniani.

Nilianza kunenepa nikiwa mdogo lakini nilitambua kwamba nahitaji kujiunga na mchezo wa kuinua vitu vizito na kuwa mtu mwenye nguvu duniani. Hivyo, niliendelea kuongeza uzito,” Hayat anasema.

“Namshukuru Mungu kwa kunipa umbo hili. Haitachukua muda kabla ya kuingia katika uwanja wa unyanyuaji vitu vizito duniani,” anasema.

Hayat, ambaye pia anajulikana kama Baba Khan, amejipatia umaarufu katika mitandao ya jamii baada ya kuweka video zenye kuonesha nguvu zake kwa kuzuia magari pasipo kutumia nguvu nyingi na au kuyainua kirahisi rahisi.

Mnyanyua vitu vizito huyo hivi karibuni alidai kunyanya kilogramu 5000 (tani 5) katika tukio lililofanyika nchini Japan mwaka 2012.

Anadai kutumia zaidi ya kalori 10,000 kwa siku ikiwamo mayai 36 kwa ajili ya kifungua kinywa, kuku wanne, kilo tatu za nyama nyekundu na lita tano za maziwa.

Tajiri huyu kutoka Mardan amekuwa akitukuzwa katika mji wake huo wa nyumbani.

Hata hivyo, watu wengi wanadai kwamba jitu hili linalofanana na hulk ni feki.

Kuna watu wengi duniani wanasema kwamba madai ya Hulk huyu wa Pakistan ni feki na kwamba uhalisia wa video zake unazua maswali mengi.

Video za Hayat, ambazo zinaonesha mtu huyo mzito akidhibiti magari kwa kutumia nguvu kidogo huku magari yakijaribu kufurukuta kuchomoka kutoka mikononi mwake bila mafanikio.

Lakini kiuhalisia nguvu kubwa inayotumiwa na magari hayo ilipaswa kukata kamba, ambazo zilichomekwa tu, lakini hakuna kitu kama hicho kinachoonekana kutokea.

Lingine linalozua maswali ni kwamba Hayat daima anaonekana kuvaa nguo za kitamaduni za jamii ya Pathani nchini humo na kujifunika kwa kashida (shali).

Hilo linampatia fursa ya kuuonesha mwili wake kuwa mnene mno kuliko uhalisia.

Madai ya rekodi yake ya kunyanyua uzito wa kilogramu 5000 haijathibitishwa popote na imedaiwa ni uongo.

“Hakuna mtu anayeweza kuvunja rekodi hii,” alisema. Baba pia alidai kwamba alipata medali kutoka WWE na jina lake liko katika Kitabu cha Rekodi za Dunia (Guinness Book of World Records. Hata hivyo madai yake hayo hayajathibitishwa.

Anasema kwamba hakuna utamaduni wa kunyanyua vitu vizito Pakistan na hivyo yeye amelenga kubadili utamaduni huo.

Wakati Hayat anadai kuwa ni mtu mwenye nguvu kuliko wote Pakistan pia anadai hana tatizo lolote la kiafya linalotokana na unene na uzito wake huo mkubwa.

Hata hivyo, kwa kuzingatia masuala ya kiafya, mnyanyua vitu vizito huyo anaweza asidumu katika ulingo wa WWE, ambako stamina ni muhimu zaidi kuliko nguvu.

Chaguo la Hayat kuwa na uzito mkubwa wa kiasi hicho, kwa mujibu ya wataalamu wa afya ni hatari na hauna afya, hata kama umelenga ubingwa wa WWE au kuweka rekodi ya kuwa mtu mwenye nguvu kuliko wote duniani.

Kuna tofauti kati ya kuwa na uzito mkubwa na kuwa mwenye nguvu na ni wazi jitu hilo la Pakistan liko mbali na ukweli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles