MANCHESTER, ENGLAND
KOCHA wa timu ya Manchester United, Jose Mourinho, amewatoa wasiwasi mashabiki wa kikosi hicho, huku akiwaambia lazima washike nafasi nne za juu kabla ya kumalizika mwaka huu.
Kabla ya michezo ya jana, Manchester United ilikuwa inashika nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi, hivyo kuwapa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo kuamini kama itaweza kufanya vizuri msimu huu.
Lakini kocha huyo mwenye maneno mengi amefunguka na kusema, lazima washike nafasi nne za juu kabla ya Januari mwakani.
“Najua tumeachwa mbali sana kwenye msimamo wa Ligi, lakini hadi kufikia mwishoni mwa Desemba ambapo hadi sasa imesalia michezo nane kumaliza mwaka, lazima tupiganie pointi 24 kama sitokuwa muongo.
“Tukiweza kushinda michezo hiyo yote, lazima tutakuwa kwenye nafasi nne za juu, ninaamini kabla ya kufikia Januari tutakuwa tumekamilisha malengo hayo,” alisema Mourinho.
Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Crystal Palace, kocha huyo alidai kuwa, ana furaha kwa kuwa asilimia kubwa ya wachezaji wake ambao walikuwa majeruhi wamepona, hivyo michezo iliyobaki atakuwa na kikosi kipana.
Miongoni mwa wachezaji hao ambao walikuwa majeruhi ni pamoja na Romelu Lukaku, Paul Pogba, Anthony Martial, na Marouane Fellaini.
Mbali na wachezaji hao kuwa majeruhi siku kadhaa zilizopita, lakini kocha huyo amekuwa na wakati mgumu kutokana na matokeo anayoyapata, huku ikidaiwa kwamba amekuwa akipishana kauli na wachezaji wake.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mtandao wa klabu hiyo, kila kitu kinadaiwa kuwa sawa na kilichobaki kwa sasa ni kuipigania timu ili iweze kufanya vizuri kwenye Ligi pamoja na michuano mingine.