28.7 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Mosul inapoisahaulisha dunia madhila ya Aleppo

Wapiganaji wa Ki-sunni wakiwa mstari wa mbele Mosul.
Wapiganaji wa Ki-sunni wakiwa mstari wa mbele Mosul.

NA RAS INNO,

KUNA mkanganyiko mkubwa unaosababishwa na kundi moja la kigaidi linalotikisa dunia kwa sasa, ambao utanzuaji wake unayahenyesha mataifa yenye nguvu za kijeshi kutokana na muktadha wa uendeshaji mapambano ya kuliangamiza kundi la dola la Kiislamu ambalo hata lenyewe pia jina lake lililogawanyika mara nne linakanganya.

IS kikiwa ni kifupi cha Islamic State, ISIL ni Islamic State International Legion na ISIS ni Islamic State in Iraq and Syria au Daesh, jina ambalo hawalipendi na wameapa yeyote atakayewaita kwa jina hilo watamkata shingo hadharani, ingawa kutimiza hilo inategemea mhanga wanayemtia mikononi mwao.

Lakini kizungumkuti kikubwa kwa sasa kuhusiana na kundi hilo ni mapigano yanayorindima katika mji wa Mosul nchini Iraq, katika kujaribu kuurejesha mikononi mwa Serikali tete ya nchi hiyo kutoka kwa wana-jihadi hao walioushikilia tangu mwaka 2014.

Kizunguzungu kikubwa zaidi ni jinsi adui mmoja (ISIS) anayepigwa vita na makundi mengi yasiyokubaliana jinsi ya kumwangamiza, anavyobadili upepo wa ufuatiliaji matukio kutoka sehemu moja kwenda nyingine kwa kadiri anavyotaka na kumwezesha kucheza turufu zake katika kuikanganya dunia.

Ni hivi karibuni tu Aleppo ilirindima kwenye vyombo vya habari kutokana na madhila ya mapigano hususani makubaliano ya usitishaji mapigano kwa muda yaliyoasisiwa na Marekani na Urusi yalipovunjika, kwa kuwa kila taifa linaunga mkono upande tofauti katika mapambano hayo yanayoangamiza raia wengi wasio na hatia hususani watoto na akina mama na kuzalisha wakimbizi wengi wa ndani na nje.

Lakini kutokana na kinachojiri sasa katika mji wa Mosul, ghafla Aleppo imekuwa kimya na haisikiki, si kwamba madhila yamekoma la hasha, yanaendelea lakini ISIL inayoshambuliwa sasa Mosul imesababisha dunia kugeuza shingo kutazama yanayotokea huko na kusahau majanga endelevu ya Aleppo.

Mji wa Mosul uliopo Kaskazini mwa Iraq ndiyo ngome iliyosalia ya IS ndani ya nchi hiyo na ikianguka mikononi mwa majeshi ya Serikali yanayotaka kuukomboa, basi inaweza kutoa fursa nzuri ya kulidhoofisha nguvu kundi hilo ingawa si rahisi sana kama inavyodhaniwa kutokana na sababu za kihistoria zilizoanza mwanzoni mwa karne ya 21.

Kwa kuwa ni eneo linalokaliwa na jamii nyingi mchanganyiko, tangu wakati huo likikusanya Waarabu, Wa-asiria, Warmenia, Waturkmen, Wakurdi, Wayazidi na jamii nyingine ndogo ndogo na wote kwa ujumla wakigawanyika katika misingi ya kiimani, ambapo Wa-sunni wamegubika zaidi lakini pia wakiwemo Wasalafi na Wakristo pamoja na Washia.

Ni mchanganyiko maridhawa wenye faida kwa upande wa magaidi, kwani mirengo ya kiimani ni nyenzo nzuri ya kuigawanya dunia na kusababisha mkanganyiko usioweza kutanzuliwa kirahisi, hivyo kuwapa nafasi ya kusimika matakwa yao kama ilivyo kwa kundi la Islamic State ingawa linasemekana kuelemea zaidi kwenye mrengo wa Ki-sunni ingawaje hulka na matendo ya kundi hilo yanalitatanisha kama kweli wanayoyafanya ni katika jina la Jihadi ya imani wanayodai kuipigania.

Lengo la kuukomboa Mosul ni jema lakini kuna changamoto nyingi hadi likamilike, mojawapo ni kuzalisha wakimbizi wapya kutoka Iraq lakini pia ushirika unaopigana kuwaondosha IS una makundi mengi yenye malengo tofauti ya kufaidika na mafanikio ya kuliondosha kundi la kigaidi la dola la Kiislamu.

Makundi hayo yanayosaidiwa na Marekani yanajumuisha majeshi ya Serikali ya Iraq yenye askari 50,000 wapiganaji wa Kikurdi wenye asili ya Peshmerga, wapiganaji kutoka makabila ya Kiarabu wenye mrengo wa Ki-sunni na wanamgambo wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia.

Kwa sasa makundi hayo kwa pamoja kwa msaada wa Marekani yanaweza kufanikiwa, lakini nini kitafuata baada ya kuliondosha kundi la ISIL mjini Mosul? Kwa sababu ni muunganiko wa makundi yanayotofautiana katika baadhi ya misingi huku kukiwa na urafiki wa mashaka, lakini kwa sasa hilo linaweza kuonekana si suala muhimu bali kuiondosha IS Mosul.

Tayari mafanikio yameanza kupatikana kwa ushirika huo kupenya katika baadhi ya maeneo ambayo awali yalikuwa ngome za ulinzi za IS ndani ya Mosul, lakini pia matokeo mabaya yameanza kudhihirika kwa maangamizi ya uhai wa binadamu kutoka kila upande unaohusika.

Wanamgambo wa Ki-sunni walioko kwenye ushirika wanawaua raia wanaowahisi kuwa wapelelezi wanaowasaidia ISIL, miongoni mwa wakazi milioni moja unusu na ushee wanaoishi Mosul.

Kwa upande mwingine IS nao wanawaua raia kwa wingi na kuwahamisha kinguvu wakiwatumia kama kinga, kati ya 1,792 waliouawa 1,120 si wapiganaji. Mamia wanakimbia na wakimbizi wa ndani wanaongezeka na kufanya kazi ya kuwahudumia kuwa ngumu katikati ya vita isiyokuwa na macho.

Hapo ndipo kiini macho cha mazingaombwe ya ISIS kinapofanyika maana kila kundi hilo likitamka ‘abracadabra uchawi tokea…!’ wanaotaka kuliangamiza hawaungani kwa mikakati ya pamoja, bali wanakurupuka na ‘abracadabra twendeni pamoja tukawapige…!’

Lakini athari kwa raia si kipaumbele chao, bali nani atakuwa na mashiko gani miongoni mwao kutokana na manufaa ya kushiriki kuing’oa ISIS. Ndiyo maana vita dhidi ya ugaidi inageuka safari ndefu isiyoleta matumaini ya kufikia hitimisho la ushindi. Ni sawa na Aleppo ilivyosahauliwa ghafla kwa ajili ya kinachojiri Mosul.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles