HASSAN DAUDI NA MITANDAO
WAJAWAZITO wametakiwa kujiweka mbali na mazingira yenye hewa chafu, ikiwamo itokanayo na moshi wa magari, ikielezwa kuwa ni sababu ya mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo.
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Aberdeen cha Scotland chini ya Profesa Steve Turner, ndio ulioibua madai hayo.
“Upekee wa utafiti wetu ni kwamba, tulitaka kujua athari anazopata mtoto endapo mjamzito anakuwa karibu na hewa chafu,” anasema Profesa Turner.
Kwa mujibu wa ripoti yake, tatizo ni gesi ya Nitrogen dioxide (NO2) inayozalishwa na vyombo hivyo vya moto, hutokana na kuungua kwa mafuta ya petroli, ingawa pia hupatikana katika moshi wa sigara.
Nitrogen dioxide huharibu ukuaji wa ‘kichanga’, hasa wiki ya 28 ya ujauzito na katika hilo, Profesa Turner anaonya kuwa huenda mtoto atakayezaliwa akawa na uzito mdogo, ugonjwa wa moyo, kisukari au pumu.
“Hivyo basi, utafiti huu unashauri kuwa jitihada zinatakiwa kupunguza hali ya akina mama wajawazito kuwa karibu na nitrogen dioxide,” anasisitiza Profesa Turner.
Kwa upande mwingine, utafiti huo uliwanyooshea kidole wajawazito wanaovuta sigara, ukidai kuwa tabia hiyo ni sehemu ya tatizo la mtoto kuzaliwa akiwa na kichwa kidogo.
Isisahaulike kuwa zipo tafiti za awali zilizowahi kuonesha kwamba hewa chafu ni chanzo cha mimba kuharibika, watoto ‘njiti’ au waliozaliwa wakiwa na uzito mdogo.
Mfano mzuri ni ule uliofanywa na Chuo cha Afya cha Royal nchini Uingereza mwaka 2016, ukiacha utafiti mwingine uliowahi kudai kuwa vipande vya uchafu hufikia mji wa mimba (placenta) wa mwanamke.
Uingereza inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Umoja wa Ulaya, ikitakiwa kuweka mikakati ya kudhibiti hali mbaya iliyopo ya uzalishaji mkubwa wa gesi ya nitrogen dioxide.
Kujaribu kukabiliana na hali hiyo, tayari Serikali ya nchi hiyo imeahidi kuwekeza si chini ya pauni bilioni 3.5 kuhakikisha inapunguza tatizo kwa kiwango cha kuridhisha ifikapo mwaka 2030.
Aidha, si tu nchini humo, hewa chafu imeonekana kuwa tatizo kubwa duniani, ikielezwa kuwa tayari imekuwa chanzo cha vifo zaidi ya milioni nane, kwa mujibu wa utafiti wa mwezi uliopita wa Chuo Kikuu cha Medical Centre Mainz.