-DAR ES SALAAM
MAANDALIZI ya mkutano mkuu wa dharura wa Kampuni ya Uwekezaji ya Nicol, yanaendelea kushika kasi huku waandaji wakisisitiza utafanyika kama ulivyopangwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa Bodi ya Nicol, Felix Mosha, alisema anasikitishwa na wanaobeza mkutano huo utakaofanyika Oktoba 12 mwaka huu, ili kuwapa fursa wanahisa kujua hatma ya fedha walizowekeza.
Alisema mkutano huo ni muhimu kwani wanahisa wa Nicol hawajakutana kwa zaidi ya miaka nane na muda wote huo wameachwa njia panda bila kujua kinachoendelea kwenye kampuni yao.
“Wanahisa wa Nicol nchini kote mjiandae kuhudhuria mkutano huo tarehe 12 Octoba 2016, katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam. Mkutano lazima ufanyike na taarifa zinazotolewa na wanaojiita menejimenti ya muda Nicol zinakwepa ukweli ambao haufichiki, kwamba zaidi ya Sh bilioni nane za wanahisa zimezolewa kutoka kwenye akaunti ya Nicol ya NMB, hivyo ni haki ya wanahisa kujua,” alisema Mosha.
Mosha aliongeza kuwa fedha hizo zimechotwa kwenye akaunti ya Nicol wakati waliozitoa hawakuwa wanaendesha kitengo chochote cha Nicol ambacho kilihitaji kuendeshwa.
Pia alisema wanaopinga mkutano huo, hawajapinga kwamba fedha zote za wanahisa wa Nicol zilikabidhiwa kwa bodi iliyokuwa anayoiongoza na hadi leo baadhi yao wanampigia simu kutaka kujua hatma ya fedha zao.
“Tatizo hili si la Mosha au wengine walioungana nami kwenye kuhoji kuchotwa kwa Sh bilioni nane. Kinachopiganiwa hapa ni amana ya wanahisa 30,000 wa Nicol au mamilioni ukiweka madhehebu ya dini, taasisi, vyama mbalimbali ambavyo vinahesabiwa kama mwanahisa mmoja kwenye hao 30,000.
“Wengi wako kwenye hali ya umasikini na kipato cha chini na kwa zaidi ya miaka mitano hawakupata gawio. Sasa watu wachache wamezoa fedha zao, zaidi ya Sh bilioni nane ambazo ndizo zingewalipa gawio, na sisi tuliokabidhiwa eti tulifumbie macho na tunaambiwa hatuna haki ya kuwakutanisha wanahisa ili waamue hatua za kuchukua kuhusu fedha zao. Hili halikubaliki,” alisisitiza.
Alisema mkutano huo utafanyika bila kuingilia uhuru wa mahakama kutokana na kesi zilizopo kwani wanahisa watajikita kwenye kujadili swala la fedha zao zaidi ya Sh bilioni nane zilizotozolewa kwenye akaunti yao.
Mosha alipendekeza kuwa katika mkutano huo, wanahisa wapewe nafasi ya kuchagua uongozi mpya, hivyo haoni sababu ya mwanahisa yeyote kupinga hoja hiyo.
“Hao wanaopinga, wanaogopa nini? Jambo zuri ni kwamba hata wale wanaopinga mkutano huo nao waje kwenye mkutano wakatoe hoja zao,” alisema Mosha.