ALIYEKUWA Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali kwa tiketi ya chama cha NCCR Mageuzi, amejiunga rasmi na Chama cha Mapinduzi (CCM) mjini Dodoma.
Machali ambaye mwaka 2010 alikihama NCCR Mageuzi na kujiunga na chama cha ACT wazalendo ambako aligombea tena ubunge na kushindwa vibaya na Daniel Nsanzugwanko (CCM) mwaka jana, alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kuridhishwa na utendaji kazi wa Rais Dk. John Magufuli.
Alisema anaridhishwa na utendaji wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa huku akiufananisha uongozi wao na wa hayati Edward Sokoine chini ya hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
“Nimeamua kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano chini uongozi wa Rais Dk.Magufuli na Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na mawaziri mbalimbali wameonyesha kutaka kufuata mwenendo wao,” alisema Machali.
Alisema serikali ya awamu ya tano imeonyesha njia katika mambo mengi na inastahili kuungwa mkono. “Ninaamua kujiunga na watu wenye mwelekeo na dhamira ya kuijenga nchi yetu kwa maendeleo enedelevu ambao ni jamii ya kinaRais Dk. Magufuli, Kassim Majaliwa,” alisema.
Akizungumzia kuondoka kwa Machali katika chama hicho, Msemaji wa ACT – Wazalendo, Abdallah Hamis, alisema:
“Tumesikia taarifa za kuondoka kwake, tunaheshimu uamuzi wake, tunamtakia maisha mema, alikuja akaziba pengo nasi tutaliziba”.
Kabla ya kuhamia CCM jana, mwanasiasa huyo machachari alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi na mafunzo wa ACT – Wazalendo
Mmoja wa marafiki wa karibu wa Machali, David Kafulila aliandika katika ukurasa wake wa Face book kwamba anampongeza mwanasiasa huyo kwa kuamua kuwa baridi kabisa kuliko vuguvugu.
“Ni hatari sana kuwa na wanasiasa au vyama vyenye misimamo vuguvugu, nusu CCM nusu upinzani. Poleni mnaoendelea kuyumbishwa na wanasiasa wa aina hii” alisema Kafulila.