25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Morocco yazindua treni yenye kasi zaidi Afrika

RABAT, MOROCCO

TAIFA la Morocco limezindua treni inayokwenda kwa kasi zaidi barani Afrika, ambayo inatarajiwa kupunguza nusu ya muda wa kilomita 200 unaotumika kusafiri katika miji ya kibiashara na kiviwanda ya Casablanca na Tangier katika safari ya saa mbili.

Uzinduzi huo umefanyika mbele ya Mfalme Mohammed VI na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ambao waliipanda treni hiyo katika safari ya kwanza kutoka Tangier hadi katika mji mkuu, Rabat.

Taarifa zinasema treni hiyo imepangiwa kwenda kwa kasi ya kilomita 320 kwa saa ikiwa ni kasi ya mara mbili zaidi kuliko treni ya mwendo kasi ya Afrika Kusini inayouunganisha uwanja wa kimataifa wa ndege Johannesburg hadi katika mji wa kibiashara wa Sandton.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari Morocco, MAP limesema kuwa mradi wa treni hiyo umegharimu kiasi cha dola bilioni 2.4, ambapo ilichukua miaka saba kuijenga reli ya treni hiyo.

Afrika inatazamia kuimarisha miundombinu ya usafiri kushinikiza biashara, uwiano na utangamano wa kieneo. Mataifa ya Afrika yanakumbatia mfumo wa reli ya mwendo kasi katika kujaribu kushinikiza na kukuza uchumi na kuimarisha kasi za kusafirisha bidhaa baina ya mataifa kibiashara.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita jitihada za kufufua mfumo wa reli umechangia baadhi ya mataifa kuamua kubinafsisha huduma hizo hususan katika mataifa ya Magharibi na Mashariki ya Afrika.

Kenya: Mradi wa reli mpya ya kisasa nchini Kenya, SGR umefadhiliwa na Serikali ya China ambao unaunganisha mji wa pwani wa Mombasa na Nairobi, ulifadhiliwa kwa mkopo wa kiasi cha dola bilioni 3 kutoka kwa benki ya China ya Exim katika kipindi cha miaka 15.

Reli hiyo ya SGR ni miongoni mwa miradi muhimu iliyoahidiwa na Rais Uhuru Kenyatta, katika kampeni za uchaguzi uliopita, ukizinduliwa mwezi mmoja kabla ya uchaguzi wa urais uliopita. Awamu ya kwanza ya reli Kenya ilianza kazi mnamo Juni 2017.

Tanzania: Jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya kwanza ya mradi mkubwa wa reli ya kisasa ya Standard Gauge liliwekwa na Rais John Magufuli, mnamo Aprili 2017. Mradi huo umenuiwa baadaye kuziunganisha nchi za Rwanda na Burundi pia.

Katika awamu hii ya kwanza, ujenzi utakuwa wa reli yenye urefu wa kilomita takribani 300, ambayo itatoka jijini Dar es Salaam na kuishia Mkoa wa Morogoro.

Ni reli ya kisasa na ya kwanza Afrika Mashariki na Kati itakayokuwa na uwezo wa kupitisha treni zitakazoendeshwa kwa nguvu ya umeme.

Reli hiyo inajengwa kwa awamu ya kwanza na kampuni kutoka nchi mbili, Uturuki na Ureno kwa gharama ya takribani dola bilioni 1.2 za Kimarekani.

Ethiopia: Reli mpya ya aina yake inayounganisha mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa na mji mkuu wa Djibouti imezinduliwa Oktoba 2016.

Reli hiyo mpya ina urefu wa kilomita 752 na inatoka Addis Ababa hadi bandari ya Doraleh katika mji wa Djibouti, kwenye ghuba ya Aden.

Sehemu kubwa ya reli hiyo imo Ethiopia, kilomita 652 kutoka Addis Ababa hadi Dewale mpakani na sehemu iliyosalia inaingia nchini Djibouti.

Gharama ya ujenzi wa reli hiyo ni dola bilioni 4 za Marekani. Ufadhili umetoka kwa benki ya Serikali ya China ya Exim na Import kwa asilimia 70 na sehemu iliyosalia kutoka kwa Serikali ya Ethiopia.

Benki ya maendeleo ya Afrika inaeleza kwamba katika ubinafsishaji, ufadhili bora, mwongozo wa sheria na utaalamu ni mambo muhimu. Mradi wa mtandao wa reli za kasi Afrika, ni sehemu ya ajenda ya Umoja wa Afrika hadi mwaka 2063 na umenuiwa kuimarisha mifumo iliyopo sasa ya kitaifa ya reli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles