Na JUDITH NYANGE,
MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella jana alilazimika kuvunja kikao cha wadau wa elimu wa mkoa baada ya wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, maofisa elimu wa msingi na sekondari kutoka baadhi ya halmashauri kutohudhuria.
Kikao hicho cha wadau wa elimu Mkoa wa Mwanza kilipangwa kufanyika kuanzia saa 2:00 asubuhi kujadili hali halisi ya elimu.
Mambo mengine ni changamoto zinazoikabili sekta hiyo na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto zilizopo na barua za mwaliko wa kikao hicho zilitolewa miezi miwili iliyopita.
Lakini hadi saa 3:18 asubuhi wakurugenzi wote wa halmashauri za wilaya za mkoa huo walikuwa hawajawasili katika ukumbi wa mikutano.
Mongella ambaye alikuwa ndiye mwenyekiti wa kikao hicho alisema ana taarifa ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga, aliyekwenda kushughulikia mgogoro wa ardhi na si wengine.
Hata hivyo aligundua kutoalikwa kwa wadau muhimu katika kikao hicho kikiwamo Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Mwanza, Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) mkoa.
Alisema wakurugenzi wengi hawakuwapo wakati maofisa elimu ya msingi na sekondari walituma wawakilishi katika kikao hicho.
Mpaka saa 3:20 asubuhi viongozi wa wilaya waliokuwapo ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dk. Leornard Masale, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Hadija Nyembo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Pendo Malabeja, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Crispin Luanda na baadhi ya maofisa elimu msingi na sekondari.