MANCHESTER, ENGLAND
KLABU ya Molde ya Ligi Kuu Norway imemtaka kocha wa muda wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, abaki England kuendelea kuifundisha timu hiyo, baada ya mafanikio aliyoyapata tangu ateuliwe kurithi mikoba ya Kocha Jose Mourinho.
Uamuzi huo unatokana na Solskjaer, kuwa msaada tangu atue Manchester United, ambapo amefikisha michezo nane bila kufungwa.
Mashabiki wa kocha huyo ambaye aliwahi kuichezea Manchester United kwa mafanikio wamekuwa na raha tangu kufukuzwa kwa Mourinho Desemba mwaka jana.
Molde ilikubali kumtoa kwa mkopo kocha huyo wakiwa katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Norway msimu huu, lakini inadaiwa kuwa wanaweza kumwachia moja kwa moja kutokana na mafanikio anayopata akiwa Manchester United.
“Nilimpigia simu mmiliki wa Molde, alinieleza Manchester United inanihitaji na ukweli ni kwamba anafahamu hii ndiyo ndoto yangu, alisema: ‘Endelea kuwa na furaha tafadhali usirudi!
“Viongozi wote wananitakia kheri hapa United, wanatambua hapa ndio nyumbani, kama nitarudi pia Molde nitafanya mambo makubwa nikiwa huko lakini itategemea,” alisema Solskjaer.
Solskjaer alikishuhudia kikosi chake kikifikisha michezo nane bila kufungwa baada ya kupata sare ya kufungana mabao 2-2 na Burnley.