Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’ na rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodgar Tenga, ni miongoni mwa majina 25 yanayounda kamati ya maandalizi ya fainali za Afrika kwa vijana walio na umri chini ya miaka 17, ambazo zimepangwa kufanyika hapa nchini mwaka 2019.
Majina hayo yalitangazwa jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
Mo, ambaye pia ni mwanachama wa klabu ya Simba, ameteuliwa kuwa mjumbe wa kamati hiyo, huku Tenga akiteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati hiyo.
Moja ya majukumu ya kamati hiyo ni kuhakikisha inafanikisha maandalizi ya fainali hizo, ambazo zitafanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Akizungumza jana wakati akitangaza majina hayo, Mwakyembe alisema, Tanzania imepewa heshima kubwa kuandaa mashindano hayo, hivyo ni muhimu kwa Serikali kushirikiana na TFF katika kufanya maandalizi ya mapema kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa Afrika.
Vigogo wengine wanaounda kamati hiyo ambayo ipo chini ya uenyekiti wa Mwakyembe mwenyewe ni Henry Tandau, ambaye ni Makamu wa Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), ambaye ameteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu.
Wajumbe wengine kwenye Kamati hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura, Mwanasheria Damas Ndumbaro, Dk. Francis Michael na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangala.
Wengine ni Aboubakar Bakhresa, Yusuph Omary, Ahmed Mgoyi, Khalid Dallah, Nasib Mbaga, Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetile Osiah, Dk. Alan Kijazi, Dk. James Dotto ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Kamishna wa Uhamiaji, Dk. Ana Peter, Fred Manoki, Lameck Nyambaya, William Erio, Kelvin Twisa, Ladislaus Matindi na Devota Mdachi.
Mwakyembe aliitaka kamati hiyo kuanza maandalizi mapema, kwavile mwaka 2019 si mbali.
“Jumamosi tutakutana tena kwa ajili ya kupanga mambo mengine na kuteua kamati ndogo ndogo za kusaidiana kwa ajili ya suala hilo na kuweka sawa mikakati mingine,” alisema Mwakyembe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe alikabidhiwa Uwanja wa Taifa, ambao ulikuwa katika matengenezo kwa takribani miezi mitatu.
Uwanja huo sasa unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia Novemba 24, mwaka huu.
Akizungumza wakati akikabidhiwa uwanja huo, Mwakyembe aliusifu kwa kusema umekuwa na mwonekano mzuri, tofauti na awali ambapo ulikuwa na vipara.
Mwakyembe alisema serikali itakabidhiwa uwanja huo ambao ulikuwa unafanyiwa marekebisho na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa ndani ya siku kumi, hivyo aliiomba TFF kwa kushirikiana na Bodi ya Ligi Kuu kuandaa mchezo mmoja wakati wa uzinduzi.
“Uwanja umekamilika na leo nimeukagua na kuridhishwa na ukarabati mkubwa uliofanywa, wameniambia baada ya siku 10 utakuwa tayari, hivyo nimewaomba TFF waangalie uwezekano wa kutafuta japo mechi moja ichezwe wakati wa ufunguzi Novemba 24,” alisema Mwakyembe.
“Kuna vijana sita wamepatiwa mafunzo ya utengenezaji wa uwanja, hivyo ni vizuri wakatumika pia katika viwanja vingine vya mikoani.
“Nawaomba Watanzania tushirikiane katika kuutunza uwanja huu, kwani gharama kubwa zimetumika katika ukarabati wake,” alisema.
Ukarabati wa uwanja huo unakadiriwa kutumia Sh bilioni 1.2.