24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Mniger Yanga afuzu vipimo

Pg 32 ANA HUSSEIN OMAR, DAR ES SALAAM

KIUNGO mpya wa pembeni wa Yanga, Issoufou Boubacar Garba, amefuzu vipimo vya afya alivyofanyiwa jana katika Hospitali ya Temeke, jijini Dar es  Salaam kabla ya kupewa mkataba wa kuitumikia klabu hiyo.

Jopo la madaktari lililoongozwa na Dk. Nassor Matuzya na mtaalamu wa viungo wa Hospitali ya Temeke, David Tesha, walisimamia kikamilifu zoezi la upimaji wa afya ya kiungo huyo ambaye amekuja nchini kusaka ulaji.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Matuzya alisema Garba amefuzu vipimo kwa asilimia 80, lakini majibu ya vipimo vingine yanasubiriwa ambapo yanatarajiwa kupatikana leo kabla ya uongozi wa klabu hiyo chini ya Katibu Mkuu, Jonas Tiboroha kumsainisha mkataba.

Kwa upande wake, kiungo huyo raia wa Niger, alisema amekuja nchini kufanya kazi licha ya kubezwa na baadhi ya vyombo vya habari juu ya uwezo wake na kusisitiza kuwa anaelewa kilichomleta na kuahidi mambo mazuri kwa mashabiki wa Yanga.

“Najua mashabiki wa Yanga wanachotaka ni ushindi na majibu yake watayapata uwanjani, kwani kila kitu kipo sawa hivyo tuombe Mungu nipate mkataba ili nianze kazi rasmi,” alisema.

Aliongeza kuwa tayari amepewa taarifa za upinzani uliopo kati ya mahasimu wa jadi Simba na Yanga, huku akisisitiza anatamani kucheza mechi hiyo ikiwa mambo yake yatafanikiwa ili awaonyeshe mashabiki wa timu hiyo uwezo wake.

“Najua kuna upinzani mkubwa wa Simba na Yanga, natamani sana kucheza hiyo mechi ili nionyeshe uwezo wangu, kwani nasikia ni moja kati ya mechi kubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati na siwezi kuwa na wasiwasi na hilo,” alisema.

Naye kocha mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm, alimmwagia sifa kibao mchezaji na kudai ni mmoja kati ya viungo bora wa kushoto aliokuwa akiwahitaji ndani ya kikosi chake ambacho mwakani kitaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika.

Pluijm alisema Boubacar ataweza kuisaidia Yanga kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira kwa kutumia miguu yote, lakini pia ana uwezo mkubwa wa kukaa na kuficha mpira pindi timu inapopanga mashambulizi langoni kwa adui.

“Boubacar ni mchezaji mzuri, naamini ataisaidia Yanga kutokana na muda mfupi niliokaa naye na kumsoma katika mazoezi, kwani ameonyesha kiwango cha juu jinsi anavyoweza kutumia vizuri mguu wake wa kushoto,” alisema Pluijm.

Wakati huo huo, Tiboroha aliliambia MTANZANIA kuwa mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo ya pande zote mbili, leo watamsainisha mkataba kiungo huyo ili aweze kuanza kazi mara moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles