WASHINGTON DC, MAREKANI
MMILIKI wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg, 33, amekubali kubeba lawama kufuatia madai kuwa mtandao wake ulieneza propaganda za chuki wakati wa kampeni za chaguzi kupitia Kampuni ya Cambridge Analytica iliyoiba taarifa za watumiaji wa Facebook kote duniani.
Zuckerberg alizungumza hayo mbele yha Bunge Marekani, akikiri kulikuwa na udhaifu mkubwa katika udumishaji usalama wa taarifa za siri za watumiaji wa Facebook.
Alisema hakujua kuwa taarifa za watumiaji bilioni mbili za mtandao huo zingevuja na kuchukuliwa na wadukuzi wa Cambridge Analytica.
“Hatukuchukua mikakati inayofaa kulinda taarifa za watumiaji wa mtandao wetu. Hilo ni kosa langu na naomba mnisamehe. Nilianzisha Kampuni ya Facebook na nalisimamia, hivyo nakubali kuwajibika,” alisema Zuckerberg.
Kampuni ya Cambridge Analytica ilishutumiwa vikali baada ya kueneza taarifa za uchochezi katika mitandao ya jamii wakati wa uchaguzi wa mwaka 2017 nchini Kenya.
Kadhalika, hali kadhalika kampuni hiyo ya Uingereza ilihusika kwa kiasi kikubwa kuvuruga chaguzi nchini Nigeria na Marekani ambako ilimsaidia Rais Donald Trump kushinda uchaguzi wa urais uliofanyika 2016.