24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TRUMP AKASIRISHWA FBI KUPEKUA OFISI ZA WAKILI WAKE

WASHINGTON, MAREKANI


RAIS Donald Trump amekasirishwa na hatua ya maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kuzipekua ofisi za wakili wake binafsi, Michael Cohen.

Stephen Ryan, ambaye ni wakili wa Cohen, amesema upekuzi huo uliofanyika juzi, ni sehemu ya maelekezo kutoka kwa Robert Mueller, mwanasheria anayeongoza uchunguzi kuhusu ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Rais Trump na Urusi wakati wa uchaguzi wa urais mwaka 2016.

Hata hivyo, gazeti la The New York Times la hapa limeripoti uvamizi huo hauhusiani na maelezo ya Mueller.

Ryan ametoa taarifa inayoeleza mteja wake tayari alishirikiana na maofisa kuwasilisha maelfu ya nyaraka kwa wachunguzi wa Bunge, ambao pia wanachunguza madai kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani.

Aidha, Ryan amekosoa uvamizi huo akisema matumizi ya vibali vya kufanyia uchunguzi hayakufuata taratibu na wala hayakuwa sahihi.

Alisema katika upekuzi huo, FBI wamechukua taarifa kuhusu matukio mbalimbali, ikiwamo nyaraka za malipo ya Dola za Marekani 130,000 yaliyotolewa kwa mcheza filamu za ngono, Stormy Daniels.

Cohen na Mueller wote hawajazungumza lolote kuhusu sakata hilo.

Akizungumza na waandishi habari, Trump amelaani vikali uvamizi huo na kusema uchunguzi unaofanywa na Mueller ni shambulizi dhidi ya Marekani.

”Nimesikia wamevamia ofisi ya mmoja wa mawakili wangu binafsi, mtu mzuri. Hali hii ni ya aibu. Ni shambulizi dhidi ya nchi yetu, kwa maana halisi. Ni shambulizi katika kile ambacho sisi wote tunakisimamia,” alisema Trump.

Katika wiki za hivi karibuni, Cohen ametawala katika vyombo vya habari tangu ilipogundulika alimlipa Dola za Marekani 130,000 Stormy kabla ya uchaguzi wa urais mwaka 2016.

Stormy alisema fedha hizo zilikuwa ni malipo ya kumnyamazisha na asizungumze chochote kuhusu madai kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Trump.

Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imeyakanusha madai ya Stormy na Rais Trump amesema hajui lolote kuhusu malipo hayo yaliyotolewa na Cohen.

Uvamizi huo ni mtihani mwingine kwa Trump wakati yeye na mawakili wake wakiangalia iwapo wakubaliane kuhusu kuhojiwa na timu ya Mueller, inayochunguza madai ya uhusiano kati ya Urusi na Marekani.

Kwa mujibu wa The New York Times, timu hiyo maalumu ya Mueller inachunguza pia malipo ya Dola za Marekani 150,000 yaliyotolewa wakati wa kampeni za uchaguzi wa urais wa Marekani kwa bilionea wa Ukraine, Viktor Pinchuk.

Fedha hizo zililipwa na mfuko wa Trump wa mradi wa mali zisizohamishika ili uweze kupewa muda wa dakika 20 kuhutubia kwa njia ya video kupitia mfumo maalumu wa kuwaunganisha watu kutoka maeneo mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles