KULWA MZEE , DAR ES SALAAM
MMILIKI wa Kampuni ya Mabasi ya Muro, Majid Kimaro, ametiwa hatiani na kutakiwa kulipa faini ya Sh milioni 115 au kifungo cha miaka minane jela baada ya kukiri kutakatisha fedha na kuongoza genge la uhalifu kuiba mafuta katika bomba linalomilikiwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Kimaro alihukumiwa jana katika Mahakama ya HakimuMkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba. Mshtakiwa alilipa faini hiyo.
Mahakama hiyo pia imeamuru gari la Scania namba T 856 ADH ambalo lilitumika kuiba zaidi ya lita 26,875.25 za dizeli na petroli litaifishwe na kuwa mali ya Serikali.
Muro alifikishwa mahakamani hapo Oktoba mwaka huu na kukaa gerezani miezi miwili ambako alifutiwa mashitaka na kusomewa upya mashitaka hayo na kuyakiri.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Simba alisema mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa makosa mawili baada ya kukiri kutenda makosa hayo mwenyewe.
Alisema katika mashtaka ya kwanza ya kuongoza genge la uhalifu, Muro anapaswa kulipa faini ya Sh milioni tano au kifungo cha miaka mitatu jela.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha, mshtakiwa atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 110 au kifungo cha miaka mitano jela.
Awali kabla ya kutolewa adhabu, Wakili wa Serikali, Simon Wankyo, akisaidiana na Jacqueline Nyantori na Patrick Mwita, waliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa washitakiwa kwa sababu makosa hayo ya wizi husababisha kuathirika uchumi na nchi kukosa mapato.
Pia aliomba gari hilo litaifishwe na kuwa mali ya Serikali kwa sababu ndilo lililotumika kubeba mafuta baada ya kulitoboa bomba na kuiba mafuta hayo.
Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 81/2018,ilidaiwa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kigamboni, Dar es Salaam na maeneo mengine, Muro akiwana wenzake ambao hawakuwa mahakamani, kwa kujua, aliongoza genge la uhalifu kwa lengo la kutoboa bomba la mafuta la TPA na kuiba mafuta kupata faida.
Muro alidaiwa katika mashtaka ya pili kuwa kati ya Julai Mosi, 2016 na Januari 8, mwaka huu maeneo tofauti tofauti wilayani Kigamboni, walipata lita 15,950.3 za dizeli na lita 10,925.22 za petroli na kusambaza mafuta hayo kwenye vituo vyake vya mafuta na kuyauza kwa watu mbalimbali .