27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, May 23, 2024

Contact us: [email protected]

MLALI: SHULE YENYE WALIMU 68, UFAULU DUNI

Shule ya Msingi Mlali

Na Ashura Kazinja, Morogoro

TUMEZOEA kusikia kuwa sababu kubwa ya wanafunzi wa shule za Serikali nchini, kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho hutokana na uhaba wa walimu, utoro kwa wanafunzi, mazingira mabovu ya kusomea na ukosefu wa vitendea kazi kama maabara na vitabu.

Ni jambo la kawaida kwa baadhi ya shule za Serikali kuwa na walimu wachache. Zipo ambazo zina upungufu mkubwa wa walimu, nyingine zina mwalimu mmoja tu, watatu na hata wawili wanaofundisha darasa la kwanza hadi la saba.

Tatizo hili limekithiri pia katika shule za msingi zilizopo wilayani Mvomero, ambapo shule ina walimu wachache ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo.

Hali hii ni tofauti kwa Shule ya Msingi Mlali, iliyopo katika kata ya Mlali ambayo ina walimu 68.

Idadi hii ya walimu inatosha kabisa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanafanya vizuri darasani kwa kuwa kila mwalimu kama atatimiza wajibu wake wa kuingia darasani kufundisha, hakuna somo ambalo litakosa mwalimu.

Lakini, jambo la kushangaza ni kwamba matokeo ya shule hii yamekuwa si ya kuridhisha kwa kuwa kila kukisha wanafunzi wa darasa la saba wamekuwa wakifanya vibaya mwaka hadi mwaka.

Shule hiyo kongwe iliyoanzishwa mwaka 1959, ina jumla ya wanafunzi 1584, hivyo kutokana na uhaba wa madarasa shuleni hapo, wanafunzi hulazimika kufika shuleni kwa zamu, ambapo wapo wanaoingia mchana na wengine asubuhi.

Akizungumzia ufaulu mdogo wa shule hiyo, Diwani wa Kata ya Mlali, Frank Mwananziche anasema shule hiyo imekuwa ikifanya vibaya kwa miaka kadhaa sasa mbali na kuwa na walimu wengi, mazingira mazuri na rafiki kwa wanafunzi kuweza kujisomea.

Mwananziche anasema kuwa jitihada za ziada zinahitajika ili kuinusuru shule hiyo iweze kufanya vema, na kwamba si jambo la kufumbia macho na la kawaida kwa wao kuwa miongoni mwa shule zinazofanya vibaya kila mwaka wakati ina walimu wa kutosha.

“Baada ya kufanya vibaya mitihani ya mwaka jana, aliyekuwa mwalimu mkuu shuleni hapo alishushwa cheo, lakini jambo la kushangaza ni kwamba mwaka huu imefanya vibaya zaidi, licha ya kuwa na walimu wa kutosha na mazingira mazuri.

“Shule ina walimu 68 na mazingira mazuri tu, hatujui tatizo ni nini. Mwaka jana aliyekuwa mwalimu mkuu aliadhibiwa kwa kushushwa cheo, sasa mwaka huu ndio wamevulunda zaidi ya mwaka jana,” anasema Mwananziche na kuongeza:

“Nashinikiza wawekeze nguvu pale, kwani kuna madarasa mawili yamejengwa kwa nguvu za wananchi lakini hadi sasa hayajaisha. Halmashauri imeshindwa kusimamia maendeleo ya shule zake.”

Anasema kuwa Serikali  inapaswa kutafuta kiini cha tatizo ili kupata ufumbuzi, kuwafukuza walimu kazi au kuwashusha vyeo si suluhisho,” anasema Mwananziche.

Naye Ofisa Elimu Maalumu wa Wilaya ya Mvomero, Stephen Msome anasema walimu wanajitahidi kuwafundisha watoto, lakini changamoto waliyonayo ni mwamko mdogo walionao jamii kuhusu elimu.

Anasema jamii inapumbazwa na masuala ya mila na desturi zao hivyo kutoipa elimu kipaumbele.

Anasema mbali na kuwapo kwa sera ya elimu bure, bado wazazi wanahofu juu ya gharama ya kuwasomesha watoto wao, hivyo kuwashawishi kufanya vibaya ili wasichaguliwe kuendelea na masomo.

“Wazazi wanaweza kuwashawishi watoto kufanya vibaya kwa kuwa hawana uwezo wa kuwapeleka sekondari, hili linatugharimu mno kiwilaya, hata elimu bure haisaidii kitu,” anasema Msome.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Evans Titi alipohojiwa kuhusu suala la wanafunzi wake kufeli anasema hana mamlaka ya kuelezea changamoto zozote zinazowakabili kwa kuwa wameamriwa kutozungumza chochote na mkuu wake wa kazi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mvomero, hadi pale atakapopata kibali.

“Jamani naomba unionee huruma, tumepewa amri ya kutozungumza chochote kuhusiana na shule zetu bila kupata kibali kutoka kwa mkurugezi au ofisa elimu wilaya, hauwezi kupata ushirikiano wa aina yoyote kutoka kwangu wala kwa walimu wengine bila ya kuwa na kibali,” anasema mwalimu huyo.

Hata hivyo, awali alijitetea kuwa si kweli kwamba huwa wanafelisha, shule yao ina mafanikio na kwamba nusu ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba mwaka huu wamechaguliwa kujiunga na sekondari.

“Diwani akisema kwamba wanafunzi wanafeli wakati nusu ya wanafunzi walifaulu, anakosea,” anasema.

Mmoja wa wananfunzi shuleni hapo, Wilson Nelson anayesoma darasa la sita, anasema tatizo linalowafanya washindwe kufanya vizuri katika masomo yao ni baaadhi yao kutopenda kujisomea na wakati mwingine baadhi ya walimu kutozingatia vipindi darasani.

Anasema walimu wapo wa kutosha lakini kuna baadhi ya masomo hawafundishwi na mengine wanafundishwa pindi inapokaribia mitihani.

Anasema kuwa jambo hilo kwa kiasi kikubwa linawafanya washindwe kuelewa kile wanachofundishwa mwishoni hivyo kuingia kwenye mitihani ya mwisho wakiwa hawajui kitu.

Naye mwanafunzi Radhia Salum anayesoma darasa la tano anasema wao hawasomi somo la Kiingereza kwa kuwa mwalimu wao alihama.

Kwa upande wao wazazi wenye watoto wanaosoma shuleni hapo, John Joel anasema hata wao hawaelewi ni kwanini watoto wao wanafeli.

“Wanafunzi hawapo vizuri darasani, lakini jambo la kushangaza ni kwamba huwa wanafaulu kuendelea na masomo ya sekondari.

“Hatujui utaratibu unaotumika kuwapeleka watoto sekondari, Baraza la Mitihani (NECTA) sijui huwa wanaangalia vigezo gani, kuna wanafunzi wajulikana kabisa kuwa hawana uwezo darasani lakini wanachaguliwa kwenda sekondari zetu hizi za kata,” anasema Joel.

Naye Fatuma Almasi anawalaumu walimu shuleni hapo kuwafanyisha wanafunzi biashara za ubuyu na kalimati darasani, jambo ambalo linawafanya washindwe kuzingatia masomo ipasavyo.

Kwa hali ilivyo, ni vema serikali na walimu kila mmoja akatimiza majukumu yake ili kunusuru hali ya elimu hususani katika shule za vijijini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles