LEONARD MANG’OHA, DAR ES SALAAM
Ni miaka 42 tangu kuanza kutumika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wadau mbalimbali wa siasa vikiwamo vyama vya siasa.
Malalamiko hayo yanadaiwa kusababishwa na kasoro mbalimbali, Katiba hiyo pia iliandika wakati mfumo wa siasa nchini ukiwa ni ule wa chama kimoja.
Baadhi ya maeneo yanayolalamikiwa ni pamoja na kupatikana kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo muundo wake utaakisi majukumu yake aidha, kwa kuwezesha kuwapo Kamisheni itakayoongoza tume hiyo katika utendaji kazi wake.
Kamisheni hiyo ndiyo itawajibika kwa mambo yote ya kisera na kimaamuzi, pamoja na kuundwa kwa sekretarieti ya tume itakayokuwa chini ya Mkurugenzi wa Tume, kama mtendaji mkuu.
Baadhi ya wanadau wanasema hili litasaidia kuifanya tume kuwa huru kwa sababu Rais anayekuwa madarakani, anaweza kuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi au anakuwa kiongozi wa chama kimojawapo cha siasa ambacho kinasimamisha mgombea, hivyo mfumo wa sasa unaompa Rais mamlaka yote ya uteuzi unakuwa na upendeleo kwa chama chake.
Baadhi ya wadau wamewahi kushauri kuwa ni vema mchakato wa kuwapata makamishna wa tume ya uchaguzi, utangazwe, ufanyike usaili kisha majina hayo yafanyiwe mchujo na kupatikana majina 20, yatakayopelekwa kwa Rais ambaye atapendekeza majina tisa yatakayopelekwa bungeni kufanyiwa uchambuzi na kujadiliwa kisha yawasilishwe tena kwa Rais ili amteue mwenyekiti wa tume.
Baada ya Rais kumteua mwenyekiti wa tume atayawasilisha majina hayo kwa Jaji Mkuu ambaye atayatangaza na kuwaapisha makamishna wa tume. Pia Rais atamteua mkurugenzi wa tume kutokana na majina mawili yatakayopelekwa kwake na tume ya uajiri wa umma kutokana na mchakato huru na wa wazi wa uajiri.
Kwa mantiki hiyo, Mkurugenzi wa Tume ndiye atakuwa mtendaji mkuu wa tume hiyo, mkurugenzi wa uchaguzi na katibu wa kamisheni ya tume (Bodi).
Kama ambavyo imekuwa Kenya upo pia umuhimu kuruhusu vyama vya siasa kuungana na kusimamisha mgombea mmoja na kutumia ilani moja ya uchaguzi bila kulazimishwa kuungana kuwa chama kimoja.
Katiba inabidi ijumuishe pia vipengele vinavyoruhusu matokeo ya urais kupingwa mahakamani kama ilivyo kwa matokeo ya ubunge na udiwani tofauti na sasa ambapo matokeo hayo hayaruhusiwi kuhojiwa baada ya kutangazwa na tume ya uchaguzi.
Kwa sababu sheria za nchi zinaitambua mahakama ndicho chombo cha mwisho cha kutoa haki, wananchi wanapaswa kupewa haki ya kuhoji. Kipengele hiki kinapaswa kuangaliwa upya, kwa sababu kinaweza kutoa mwanya kwa tume kumtangaza mtu kwa masilahi binafsi hata kama hakushinda na kupoteza haki ya walio wengi.
Mathalani kukiwa na kikundi cha watu wenye nia ovu, wakaamua kumpenyeza mtu kwa masilahi binafsi katika mchakato wa kumpata mwenyekiti wa tume na kwa bahati mbaya mamlaka ya uteuzi isiligundue hilo ni wazi kuwa taifa linaweza kutangaziwa Rais ambaye hajachaguliwa kwa kura nyingi.
Mabadiliko mengine yanayopaswa kufanyika ni kuitaka NEC kusimamia uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais kwa sababu ndicho chombo chenye utaalamu na weledi wa kusimamia uchaguzi.
Kitendo cha uchaguzi mdogo kusimamiwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kunaleta hisia za unyonge kwa vyama ambavyo havijashika dola na kuvifanya kuamini kuwa havitendewi haki.
Hivi karibuni limezuka balaa la wabunge kuhama vyama vyao na kujiunga na vyama vingine, hasa wapinzani kuhamia chama tawala, hali hiyo inasababisha kurudiwa kwa uchaguzi katika majimbo na kata na kuligharimu Taifa fedha nyingi, ni vema mabadiliko yatakayoruhusu mbunge kuhama bila kuhitajika uchaguzi wa marudio.
Mabadiliko mengine yanayopaswa kufanyika ni pamoja na kumruhusu mbunge ama diwani aliyepo madarakani kuendelea na uongozi hadi hapo kipindi chake kitakapofikia ukomo, endapo atafukuzwa uanachama na chama chake na hii inaweza kuwa rahisi zaidi ikiwa mfumo wa mgombea binafsi utaruhusiwa.
Kwa mbunge au diwani anayehama chama chake atalazimika kuuvua ubunge na nafasi yake kuchukuliwa na mgombea aliyeshika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita.
Mabadiliko haya yanapaswa kwenda sambamba na kizuizi cha kisheria kinachomzuia mtu anayejivua uanachama wa chama chake kwa makusudi kutogombea katika eneo hilo au jingine lolote kwa angalau vipindi viwili mfululizo. Kwa mantiki hiyo, uchaguzi utarudiwa pale tu kiongozi wa eneo husika amefariki dunia.
Kwa Katiba ya sasa ambayo imejaa viraka si rahisi kuyajumuisha yote haya badala yake ni vema kuandikwa Katiba mpya, ambayo hata hivyo mchakato wake umekwama tangu mwaka 2014 uliposimama, huku Serikali ikieleza kutokuwa na nia ya kuendelea na mchakato huo kwa sasa.
Licha ya msimamo huo wa Serikali viongozi wa upinzani wameendelea kuomba mchakato huo uendelee ili kupata uwanja huru wa siasa.
Mapema wiki hii muungano wa vyama vya upinzani kupitia kwa Mwenyekiti wa Chama United Peoples Democratic Party (UPDP), Fahim Dovutwa, amesisitiza uhitaji mjadala wa Katiba, ambao pamoja na mambo mengine utawezesha kupatikana kwa dira ya Taifa kwani iliyopo haitekelezeke, jambo linalofanya kila rais anayeingia madarakani anakuja na mambo yake
Dovutwa anasema kupatikana kwa Katiba mpya pamoja na mambo mengine itasaidia kuondoa kero za Muungano ambazo licha ya kudumu kwa miaka 55 tangu kuasisiwa baadhi ya mambo wanaendelea kusuasua.
“Watwambie wanataka tena miaka 55, haya maneno changamoto, kero ni lugha zinazopoza mambo yaonekane kuwa ni madogo, tulitarajia miaka hii 55 wangetuambia wamemaliza kero zote.
“Ili kulimaliza jambo hili tunahitaji mjadala wa Katiba, ili pia tutunge dira ya Taifa kwa sababu dira iliyopo haitekelezeke, kila mmoja akija anakuja na mambo yake” anasema Dovutwa.
Mchakato wa Katiba mpya ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne umekwama tangu mwaka 2014, baada ya Bunge Maalumu la Katiba, kutawaliwa na hoja ya muundo wa Serikali. Baadhi ya wajumbe wakitaka kuwapo kwa Serikali mbili, wengine kutaka Serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Kwa muktadha huo ipo haja ya kupatikana kwa Katiba mpya ili kuondokana na malalamiko hayo na mengine.