30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 31, 2023

Contact us: [email protected]

Tatizo kwa Ramaphosa ni ANC

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

NI miezi 15 tu imepita tangu alipoingia madarakani kukikalia kiti cha Jacob Zuma aliyejiuzulu na sasa Rais Cyril Ramaphosa anakabiliwa na changamoto ya kuingia Ikulu kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi wa Afrika Kusini katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Mei 8, mwaka huu.

Zuma, ambaye Ramaphosa alikuwa makamu wake kwa kipindi cha miaka minne, aliachia ngazi mwanzoni mwa mwaka jana, ingawa kwa wachambuzi, lengo lilikuwa ni kukisaficha Chama tawala, African National Congress (ANC), kilichoonekana kupoteza mvuto kutokana na kashfa za rushwa.

Haijasahaulika kuwa kipindi hicho kilishapoteza viti vingi katika Uchaguzi Mdogo wa mwaka 2016 na tafiti hazikuficha kuwa umaarufu wa ANC ulishuka hadi asilimia 54, ikitabiriwa kuwa ingefikia asilimia 50 mwaka huu endapo kiongozi huyo angebaki Ikulu.

Kwa kipindi kifupi alichokaa madarani, Rais Ramaphosa ameweza kusimama imara kukabiliana na upinzani wa kutosha kutoka kwa vyama viwili; Democratic Alliance (DA) na Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema.

Licha ya kuingia madarakani akikabiliwa na mzigo mzito wa kuisaficha ANC iliyochafuliwa na miaka tisa ya uongozi wa Zuma, ni wazi Ramaphosa ana kila sababu ya kujivunia kuelekea Uchaguzi Mkuu wa wiki ijayo, hilo likithibitishwa na  utafiti wa hivi karibuni.

“Tunakwenda katika uchaguzi na sijui matokeo yatakuwaje lakini nakwenda nikiwa najiamini sana… Najua nitaibuka na ushindi mnono,” anasema Ramaphosa.

Majibu ya utafiti yameonyesha kuwa anakwenda kwenye uchaguzi akiwa kifua mbele kwani anakubalika kwa asilimia 60, akiwaacha mbali wapinzani wake, Mmusi Maimane wa DA asilimia 42 na Malema asilimia 38. Mwaka jana, utafiti mwingine wa Chuo Kikuu cha Johannesburg ulionyesha kuwa asilimia 55 ya watu 3 431 walikuwa na imani na Ramaphosa.

“Cyril Ramaphosa alipoingia madarakani tu, nilianza kugundua kuwa kuna mabadiliko yatatokea. Ni rahisi kumwamini, ni tofauti na Zuma. Aliposema anataka kujenga nyumba, wala sikuwa na shaka naye, nilisema atafanya hivyo.” anasema Tshepo Dichaba mwenye umri wa miaka 19, ambaye ni kinyozi mjini Alexandra.

Tukio lililoonekana kuwavutia wengi ni lile la Rais Ramaphosa kusitisha mkutano wake wa kampeni na kukimbilia mjini Alexandra ambako kulikuwa na maandamano ya kulalamikia hali ngumu ya maisha, jambo lililoonekana kuwakuna wengi.

“Ramaphosa ni bora kuliko Zuma. Wakati wa Zuma, ni rushwa tu. Kipindi kile matatizo matupu. Kwa sasa mambo mazuri.” anasema mwananchi mwingine, Thomas Lidebawe (64)

Hata hivyo, wakati mambo yakionekana kuwa mazuri kwake, bado wachambuzi wanaiona ANC kuwa ni tanuri kwa Rais Ramaphosa hata kama atashinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Tangu mwaka juzi, kumekuwapo na mpasuko ndani ya chama hicho, chanzo kikubwa ikiwa ni baadhi ya vigogo, ambao ni rafiki wa Zuma, kutoridhishwa na kitendo cha Ramaphosa kukikalia kiti cha urais.

Kuna shaka kuwa wengi wao wanashikilia nyadhifa za juu ndani ya ANc, wakiwa na utajiri na nguvu kubwa ya ushawishi, hivyo huenda wakamwangusha Ramaphosa wakati wa kura za ndani ya chama mwaka 2022, kwa maana ya kumzuia kumalizia awamu yake ya pili madarakani.

Akilizungumzia hilo, mchambuzi wa siasa kutoka Chuo Kikuu cha Free State, Sethulego Matebesi, ambaye anaamini Ramaphosa ndiye rais bora kuwahi kutokea nchini Afrika Kusini tangu kuondoka madarakani kwa mzee Nelson Mandela mwaka 1999, anasema:

“Hatari iliyopo haitatokana na uchaguzi huu (wa mwaka huu). Hatari ya Afrika Kusini ni kile kitakachotokea katika uchaguzi wa ndani wa ANC. Hakuna uhakika kwamba Cyril Ramaphosa atarejea baada ya miaka mitano kumalizia awamu yake ya pili.”

Hakuna siri kwamba uteuzi wa Barala la Mawaziri lake lililowatema vigogo 13 waliokuwa wakifanya kazi chini ya Serikali ya Zuma ulimuongezea maadui kwa kiasi fulani ndani ya ANC, ikielezwa kuwa hata Zuma anacheza kiaina kila ya mlio wa ngoma anaousikia ANC kupitia kwa vibaraka wake wanaoendeleza mapambano ya chini kwa chini dhidi ya Ramaphosa.

Si tu kukabiliana na wabaya wake ndani ya ANC, pia Ramaphosa anakabiliwa na mtihani mzito wa kuitambulisha upya taswira ya chama hicho kwani tayari kimeonekana kupoteza ushawishi wake mbele ya wananchi walio wengi.

Mfano mzuri katika hilo ni kile alichokisema mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Jacob Mpho (34). ambaye hakuficha kuwa atakwenda kupiga kura kwa ajili ya Ramaphosa tu na si mapenzi yake kwa ANC.

Utafiti wa Taasisi ya IRR (Institute of Race Relations) umeweka wazi kuwa ushawishi wa ANC kuelekea Uchaguzi Mkuu umeshuka kwa asilimia 11, ingawa bado kimeendelea kuwa juu ya DP na EFF.

Kwamba ANC itaambulia asilimia 51 ya kura zote, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2014, ambapo iliweza kuibuka na ushindi mnono wa asilimia 62.15.

“Kufikia Desemba (mwaka jana), kwa msaada wa Cyril Ramaphosa, ANC imeweza kurejesha kwa kiasi fulani imani iliyokuwa imepotea chini ya Jacob Zuma. Hiyo imetokana na mambo mawili aliyofanya Ramaphosa: Uongozi bora na ukali wake dhidi ya vitendo vya rushwa,” inaeleza ripoti ya utafiti huo.

Mbunge wa Chama cha DA, Makashule Gana, aliongeza kuwa rushwa na ahadi zisizotimia wanazopewa wananchi ndiyo sababu ya ANC kupoteza ushawishi wake. “… Tatizo la ANC si Jacob Zuma. Ni taasisi yote kwa ujumla wake. Mwaka 1994, tulimpigia kura Nelson Mandela, halafu akaja Thabo Mbeki, halafu Jacob Zuma lakini  hakuna yeyote aliyeleta mabadiliko,” anasema Aubrey Kutlawano, mwananchi aliyehudhuria mkutano wa kampeni za Rais Ramaphosa.

Kutlawano mwenye umri wa miaka 42 anaongeza kuwa uamuzi wake ni kutopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwani haoni faida yake. “Ni watu wanaofanya kazi kwa ajili ya matumbo yao,” anasisitiza.

Katika hatua nyingine, suala la watuhumiwa wa rushwa kutohukumiwa nalo limekuwa likilalamikiwa. Ni kama alivyosema mpinzani mkubwa wa Ramaphosa katika Uchaguzi wa mwaka huu ambaye anakiwakilisha Chama cha DA, Mmusi Maimane. “Tunasema wazi kabisa, hatuwezi kuishi katika nchi ya rushwa na hakuna anayehukumiwa,” anasema.

Itakumbukwa kuwa kauli hiyo ya Maimane wakati wa kampeni, ikimlenga Katibu Mkuu wa ANC, Ace Magashule, ambaye anatajwa kujihusisha na rushwa.

“Kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu sasa, tulifungua mashitaka dhidi ya Magashule… Waafrika Kusini hawawezi kupigia kura wala rushwa…” aliongeza Maimane.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles