BRIGHITER MASAKI
Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Udunga, amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujikwamua kiuchumi na kuwa chachu maendeleo katika Taifa.
Akizungumza wakati wa kufunga kongamano la makambi ya dhehebu la Adventista Wasabato leo Jumamosi Julai 13, jijini Dar es Salaam Udunga amesema kijana yeyote anatakiwa kufanyakazi kwa bidii ili aweze kumtumikia Mungu kikamilifu.
“Kijana yoyote lazima awe na kazi ya kufanya, ndiyo sababu kubwa hata hapa kanisani huwa tunatoa elimu ya ujasiriamali, hata vitabu vya dini vimeandika asiyefanya kazi na asile, na kwa wenzetu waislamu pia wanazo nguzo tano, lazima kusali, kutoa sadaka pamoja na kwenda kuhiji huwezi kwenda kuhiji kama hauna pesa,” amesema Udunga.
Naye Mchungaji, Kibunto Daniel, amesema kongamano hilo la wiki nzima la mwaka huwakutanisha waumini wa dhehebu hilo na madhehebu mengine kusherekea na kujifunza neno la Mungu na fursa mbalimbali bila kujali dini au kabila gani mtu anatoka.
“Mikutano hii huwa inachukuwa watu wa namna yoyote kwa sababu ndani yake siyo tu kwamba huwa kuna neno la Mungu kunakuwa na warsha mbalimbali ndani yake kunakuwa na semina za ndoa, uhusiano wa vijana na uchumba” amesema Daniael.
Kwa upande wake Mchungaji, Ezekia Chabuma, aliishukuru Serikali kwa kuwezesha kuwapo mazingira yanayoruhusu mikutano ya dini kufanyika na kwamba mkutano huo umewezesha kutoa mafunzo kuhusu namna bora ya kuishi katika ndoa.