25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Maajabu shule za kata

*Kati ya shule 100 bora, 52 ni za kata, Walimu waeleza siri ya kufanya vizuri licha ya kuwa na changamoto lukuki, nyingine zina mazingira magumu ambayo wanafunzi wakifika na kuona hukimbia, baadhi zina upungufu wa walimu, nyumba za walimu

ANDREW MSECHU NA ELIZABETH HOMBO – Dar es Salaam

KWA miaka mingi shule za binafsi na zile za seminari, zimekuwa zikifanya vyema katika mitihani ya taifa, jambo ambalo limepinduliwa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita mwaka huu kwa shule za umma kufanya vizuri zaidi.

Katika shule hizo za umma, mbili za kata ziliingia kundi la shule 10 bora kitaifa.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) Julai 1, kati ya shule 10 bora kitaifa, nne ni za Serikali na katika kundi la shule 100 bora, 64 ni za Serikali ambazo kati yake 52 ni za kata.

Katika mahojiano na MTANZANIA Jumapili, wakuu wa shule za kata za Kisimiri na Muriet za mkoani Arusha ambazo zimeingia 10 bora, walieleza mazingira magumu ya shule zao na jinsi wanavyoyageuza kuwa fursa.

Wamezungumzia changamoto zinazowakabili ambazo wakati mwingine hufanya wazazi kutopeleka watoto wanaochaguliwa kujiunga kidato cha tano.

Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisimiri, Fidelis Tyanja, alisema wao hawashindani na shule yoyote, lakini lengo lao ni kuhakikisha wanazalisha wanafunzi bora na kupata daraja la kwanza pekee.

Alisema mazingira ya shule hiyo ni magumu na wanafunzi wengi wanaopangiwa shuleni hapo wamekuwa hawaripoti, lakini walimu wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha wale wanaokubali kujiunga nao wanakuwa bora.

“Kwetu sisi mazingira hapa ni magumu sana. Lakini tunahakikisha tunawafundisha vizuri watoto kwa sababu nchi inawahitaji, tunawasaidia kwa kiwango cha juu, tunajituma hasa. Tukifika hapa tunatumia muda wetu wa ziada kuwasaidia.

“Lengo letu siyo kushika nafasi ya kwanza, ila tunalenga kupata wanafunzi bora. Hata kama tukishika nafasi ya 100, tunachojali ni kuwa tunatoa wanafunzi bora na kuhakikisha wote wanapata daraja la kwanza,” alisema Tyanja.

Alisema japokuwa mazingira ya Kisimiri ni magumu, lakini hawatarajii kushuka kwa kuwa wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wao wanakuwa wa kiwango cha juu kitaaluma.

Tyanja alieleza kuwa kutokana na ugumu wa mazingira, wanafunzi wengi wanaopangiwa hawaripoti shuleni na wengine wamekuwa wakifika na baada ya kuona hali ilivyo huondoka.

Alisema wanafunzi waliomaliza kidato cha sita mwaka huu walisajiliwa 115, lakini walioendelea na masomo shuleni hapo ni 60 pekee na wengine walikataa kujiunga na shule hiyo baada ya kufika na kuona mazingira magumu.

“Kwa mwaka huu, wanafunzi waliopangiwa kujiunga na shule hii kwa kidato cha tano ni 167, lakini hatutarajii kuwa wataripoti wote. Wengi wanafika hapa, lakini wakiangalia tu mazingira wanageuza na kundoka, hawarudi tena,” alisema.

Shule hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa walimu wa sayansi, lakini kwa kushirikiana na wazazi, wameajiri walimu sita wa masomo hayo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwandet iliyopo mkoani Arusha, John Masawe, alisema shule hiyo ambayo imekuwa ya nne kitaifa, kwa mara ya kwanza ilitoa wanafunzi wa kidato cha sita mwaka jana.

Alisema mwaka huo hawakusomeka vizuri kitaifa kwa sababu walikuwa na jumla ya watahiniwa 29, ambao 16 kati ya hao walipata daraja la kwanza na pili huku 13 wakipata daraja la tatu.

“Mwaka jana hatukusomeka vizuri kitaifa kwa sababu tulikuwa na watahiniwa chini ya 30,” alisema.

Alisema mwaka huu walipata watahiniwa 77 na baadaye mmoja ambaye alikuwa akishika nafasi ya kwanza darasani alipata ujauzito wakamwondoa shuleni.

“Tukawa na watahiniwa 76 ambao waliopata daraja la kwanza walikuwa 70, huku sita wakipata daraja la pili.

“Siri ya kufanya vizuri tuna mikakati yetu, tulitaka shule ijulikane kwa kuwa na matokeo mazuri. Huwa tuna vipindi vya kawaida darasani, pia wanafunzi wanafanya ‘discussion’ na ‘topic’ huwa tunazimaliza mapema, pia tunakuwa na ziara za mara kwa mara kwa kutembelea shule mbalimbali,” alisema.

Akizungumzia changamoto zilizopo shuleni hapo, alisema hakuna nyumba za walimu kwa sababu eneo hilo ni la wafugaji.

“Walimu wanatokea mbali kwa sababu eneo shule ilipo ni la wafugaji na barabara inayoelekea shuleni ni mbovu,” alisema mwalimu Masawe.  

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Chrisdom Mwaisela, alisema anashukuru kwa hatua ya shule yake kupata mwanafunzi bora aliyeongoza katika masomo ya biashara, akisisitiza kuwa mambo hayo hayaji kama miujiza, bali ni kwa juhudi na malengo.

Alisema matokeo ni mazuri na kwamba shule yake ndiyo inayoonekana kuongoza kwa kuwa na wanafunzi 142 wenye daraja la kwanza, hatua iliyoongeza furaha miongoni mwa walimu na wanafunzi.

“Ukiangalia pia tumetoa wanafunzi bora 10 katika maeneo tofauti, ukweli ni kwamba maandalizi haya ni ya muda mrefu. Tumekuwa tukijitahidi kusimamia nidhamu, lakini zaidi walimu wamekuwa wakijitahidi kumaliza silabasi mapema na kuwapa wanafunzi muda mrefu wa mazoezi na mitihani.

“Tumekuwa tukisimamia nidhamu tangu wanafunzi wanapofika shuleni, lakini walimu nao wamekuwa wakisimamiwa ipasavyo kuhakikisha wanatekeleza vyema wajibu wao.

“Kwa mfano, kwa sasa wanafunzi wa kidato cha nne walishamaliza silabasi zote na wakati wenzao wakiwa likizo, wenyewe walibaki shule kwa siku mbili kwa mazoezi na mitihani,” alisema.

Alieleza kuwa katika maandalizi ya kufanya vizuri, wanafunzi wa kidato cha nne ambao tayari wameshamaliza topiki zao.

“Wakirudi sasa hivi wanakuwa wanafanya marudio katika maeneo magumu, mazoezi na mitihani ya kujiandaa kwa mtihani wa mwisho, kwa hiyo uwezekano wa kufanya vizuri ni mkubwa,” alisema.

JAFO: SHULE ZA SERIKALI ZIMEFANYA MAPINDUZI

Akizungumzia matokeo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema matokeo ya mwaka huu yameonesha azma ya Serikali kufanya mapinduzi katika sekta ya elimu

Alisema matokeo hayo yameweka historia kwa shule za Serikali tofauti na miaka ya nyuma ambapo zilizoeleka kufanya vibaya.

Jafo ambaye wizara yake ndiyo yenye dhamana ya kuhakikisha shule za Serikali zinakuwa na walimu na miundombinu bora, alisema kutokana na matokeo hayo, ni vyema wazazi wakaacha kasumba ya kuhamisha wanafunzi wanaofaulu kidato cha nne na kupangiwa kwenye shule hizo.

Alisema tathmini yao inaonesha kati shule 10 bora kitaifa, nne ni za Serikali na mbili kati yake zikiwa za kata.

Shule hizo na nafasi zake kwenye mabano ni Shule ya Kisimiri (1), Mwandeti (4), Tabora Boys (5) na Kibaha (6).

“Haya ni mafanikio ya safari ambayo tumeamua kuifanya. Kihistoria shule hizi za Serikali zilikuwa hazionekani. Hili ni jambo la kihistoria sana limetokea nchini kwetu,” alisema Jafo.

Alisema pia kuwa katika orodha ya shule ya 11 hadi 20, Serikali imeingiza sita ambazo ni Iliboru (11), Nachikwea (12), Mzumbe (13), Mwanamwema (14), Tabora Girls (15) na Dareda (16).

“Kwetu ni jambo la kishtoria kuona shule za Serikali zinafanya vizuri. Miaka minne iliyopita ukizungumzia shule 100 bora unatafuta za Serikali zimedondokea wapi, lakini mwaka huu katika shule 100 bora, 64 ni za Serikali kati yake 52 ni kata na 12 ndiyo zile kongwe na vipaji maalumu.

“Haya ni mapinduzi makubwa, wengine walikuwa wakizibeza hizi shule, na huu ni ujumbe kwamba kwa wale wazazi ambao matokeo ya kidato cha nne yakitoka wanakimbilia shule zenye jina maarufu, sasa waacheni watoto huko kwenye shule za kata watulie wasome,” alisema Jafo.

SHULE KUMI BORA KITAIFA

Shule kumi bora kitaifa ni Kisimiri (Arusha), Feza Boys (Dar es Salaam), Ahmes (Pwani), Mwandet (Arusha), Tabora Boys (Tabora), Kibaha (Pwani), Feza Girls (Dar es Salaam), St. Marys Mazinde Juu (Tanga), Canossa (Dar es Salaam) na Kemebos (Kagera).

SHULE KUMI ZA MWISHO

Shule kumi za mwisho ni Nyamunga (Mara), Haile Selassie (Mjini Magharibi – Unguja), Tumekuja (Mjini Magharibi – Unguja), Bumangi (Mara), Buturi (Mara), Mpendae (Mjini Magharibi – Unguja), Eckernforde (Tanga), Nsimbo (Katavi), Mondo (Dodoma) na Kiembesamaki A Islamic (Mjini Magharibi – Unguja).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles