32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkuu wa Majeshi awapa somo viongozi wa dini

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

MKUU wa Majeshi yaUlinzi, Jenerali Venance Mabeyo, amewataka viongozi wa dini kutii mamlaka bila kujali wana elimu kiasi gani.

Suala hilo ni miongoni mwa changamoto tano alizoziainisha wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Halmashauri ya Walei Tanzania katika viwanja vya Msimbazi Center, Dar es Salaam jana.

“Ushirikiano na heshima ni muhimu katika kulinda na kudumisha nidhamu ya kanisa.

“Ni wajibu wa kila kiongozi kutambua kwamba haijalishi amesoma sana, bado anao wajibu wa kutii mamlaka, haya yakifanyika vema kanisa litasonga mbele kwa nguvu,” alisema.

Jenerali Mabeyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, pia alisisitiza jitihada zifanyike ili kanisa lisionekane linapigia chapuo mambo ya fedha kuliko masuala ya kiimani.

Alisema elimu ya utoaji inatakiwa izingatie kumpa mwanga muumini kumjua Mungu na kumpenda ndipo suala la kumtumikia litafanyika kwa umakini na urahisi.

“Muumini afundishwe kwanini anatoa na kuna faida gani, na asipotoa anapata faida gani kiroho na kimwili.

“Uwepo uwazi wa kutosha katika mapato na matumizi ya fedha, yale yanayojitika kwa maendeleo ya kanisa na kuwapa waumini moyo wa kutoa zaidi kwa sababu wanaona mambo mema na mazuri yanayotokana na utoaji wao,” alisema.

Jenerali Mabeyo alisema pia uhaba wa elimu na mafunzo ya kutosha juu ya uongozi wa kanisa umesababisha wengine kuongoza parokia au chama cha kitume kama wanavyoongoza katika sehemu zao za kazi na kuhimiza kuwepo kwa semina za mafunzo juu ya uongozi wa kanisa.

Alisema kanisa limepiga hatua kubwa na kumekuwa na maendeleo ya kiroho na kimwili katika nyanja zote yaliyochangiwa kwa kiasi kikubwa kupitia walei.

“Kanisa limeshuhudia mwamko wa kujitolea kwa waamini katika kazi za maendeleo ya kanisa hususani ujenzi wa makanisa, nyumba za mapadri na uimarishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

“Dhana ya kutegemea misaada toka nje ni wazi kwamba haipo tena kwa waamini, wamisionari wa nyakati za sasa ni sisi wenyewe.

“Jimbo Kuu la Dar es Salaam ni mfano halisi wa namna walei wanavyojitolea na kujenga makanisa mapya na kuyakarabati ya zamani, kujenga nyumba za mapadri na za watawa,” alisema.

Katika sherehe hizo, Jenerali Mabeyo pia alizindua kitabu chake kijulikanacho kama ‘Wewe ni shahidi wa kristo’.

ASKOFU PENGO

Naye Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, akihubiri katika shehere hizo, alisema umefika wakati waamini kuwa kitu kimoja.

“Tujirudi na kuwa kitu kimoja, kama ambavyo tumefundishwa katika utatu mtakatifu… yaani baba, mwana na roho mtakatifu,” alisema.

Alisema kazi ya walei ni ya kujitolea, hivyo si ya kuajiriwa kama mtu anakwenda serikalini kutafuta ajira.

“Watu wamefanya eneo hili kama la kutafuta kazi serikalini, sisi kwa walei ni wa kujitolea, tuepuke mambo ambayo si mazuri… katika ulimwengu huu binadamu tumekuwa wa kutafuta zaidi si kwa kutafuta kwa ajili ya wengine,” alisema Askofu Pengo. 

RAIS TEC

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga, alisema dunia inasumbuliwa na uovu wa aina mbalimbali na ushiriki wa walei ni muhimu katika kuzuia mabaya.

“Dunia inasumbuliwa na uovu kama vile utesaji wa kikatili, mauaji ya watu, utekeaji nyara, ukandamizaji wa wanyonge, ukiukwaji wa haki za watu, unyanyasaji wa kijinsia, ukengeufu wa mahusino ya mapenzi, uharibifu wa mazingira na uharibifu wa uhai wa binadamu.

“Katika kuendeleza au kuzuia mabaya ushiriki wa walei ni mkubwa,” alisema Askofu Nyaisonga.

Kuhusu maadhimisho hayo, alisema walei walipitia misukosuko mingi, lakini uamuzi wao wa busara unawafanya wastahili pongezi.

“Baraza tunaona mnastahili pongezi kwa kufikia jubilei hii, huku utume wenu ukiwa imara, mmeshiriki misukosuko mingi ya kisiasa, kiuchumi na kiimani, bila maamuzi ya busara mngeweza kulitumbukiza taifa kwenye migogoro na hata machafuko makali,” alisema.

MWENYEKITI WALEI

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Taifa, Gasper Makiluli, alisema ilianzishwa mwaka 1969 kwa lengo la kushirikiana katika shughuli za kanisa.

“Kwa ushirikiano mzuri tumepata fursa ya kushiriki katika ujenzi wa vituo vya sala, tunaona idadi kubwa ya vyama, mashirika na jumuiya za kitume vikianzishwa na kuimarika.

“Kumekuwa na ongezeko la hari ya walei katika kutumia uwezo wao kulijenga kanisa,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuna changamoto kadhaa kama upungufu wa huduma za kiroho na malezi ya kiimani kutokana na upungufu wa mapadri baada ya kuongezeka kwa vituo vya sala, vigango na parokia.

Changamoto nyingine alisema ni uharibifu wa imani kutokana na utandawazi na kusababisha baadhi ya waamini kuvaa nguzo zisizo za heshima, mmomonyoko wa maadili kuongezeka kwa kasi kubwa katika familia na uchumba sugu kwa vijana wengi.

Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salam, Kardinali Pengo, pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, na Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali, Martin Busungu.

Wengine ni Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Wanamaji, Meja Jenerali Richard Makanzo, Kamishna wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda na Rais mstaafu wa Bunge la Afrika, Dk. Getrude Mongela.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles