23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi NEMC atembelea mradi wa bomba la mafuta

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MKURUGENZI Mkuu wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka, amefanya ziara katika eneo linalotarajiwa kujengwa mradi wa kituo kitakachopokea na kuhifadhi mafuta katika Kijiji cha Chongoleani, Tanga.

Lengo kuu la ziara hiyo ni kukagua utekelezaji wa sheria, taratibu na kanuni za utunzaji wa mazingira katika hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi huo.

“Sisi kama NEMC ni lazima tutimize maagizo ya Mheshimiwa Rais  Samia Suluhu Hassan na moja ya mikakati ambayo tumeiweka ni kuanza kuwa na mtazamo chanya kwa maana ya kwamba wawekezaji wote hasa kwenye miradi ya kimkakati tunatakiwa kuwa nao kuanzia hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi ili kutambua nini wanakifanya na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhakikisha wanaenda sambamba na Sheria ya Mazingira.

Eneo ambalo uwekezaji wa bomba la mafuta unafanyika. NEMC ilifika kwa ajili kuangalia utekelezaji
wa Sheria ya mazingira wakati mradi huo ukiwa katika hatua za awali.

Dk Gwamaka amesema mradi wa bomba la mafuta ni  moja ya mkakati katika nchi utakaoleta tija na faida.

Aidha amewapongeza viongozi wa mradi wa EACOP kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kushirikiana na jamii inayozunguka mradi ikiwa ni pamoja na kuwalipa fidia na kuwashirikisha katika kila hatua.

Naye Ofisa Mazingira kutoka NEMC, Dalia Charles ametoa rai kwa wananchi wa Chongoleani na nchi kwa ujumla kuwa Baraza limejiridhisha na mikakati mahsusi iliyowekwa na wawekezaji kudhibiti mwanya wowote wa athari inayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chongoleani, Mwaveso Mbega ameuhakikishia umma kuwa mradi huo umepokelewa vizuri na wananchi wa Kata hiyo ambao wameridhika kuachia maeneo yao ili ujengwe na kuishukuru Serikali kupeleka mradi katika eneo hilo.

Amewaomba wananchi wa Chongoleani kuwa na imani na mradi huo kwani Serikali ina nia njema na haiwezi kupeleka mradi wenye madhara, kwani unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Naye Mtendaji wa Kata hiyo, Mohamedi Salimu amesema kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya wawekezaji na wananchi wanaozunguka mradi huo, ikiwamo kupata stahiki zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles