24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi IMF aiona Tanzania inavyopiga hatua kukuza uchumi

Galila Wabhanh’u

MIAKA minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli na safari ya Tanzania ya viwanda inaendelea kuonekana kwa vitendo.

Rais Dk. Magufuli ametimiza maoni na shauku ya Waafrika kuona nchi kama Tanzania zinapiga hatua kiuchumi. 

Ninakumbuka Christine Largade, alihojiwa kuhusu ni nchi gani Afrika inaweza kuwa na uchumi mzuri, alitoa maoni yake akiwa makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU) pale Addis Ababa nchini Ethiopia.

Christine Largade ambaye si tu  ndiye mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Mkurugenzi wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (International Monetary Fund-IMF), lakini pia ndio Mkurugenzi wa kwanza wa shirika hilo katika miaka 72 ya uhai wa IMF  kutembelea Addis Ababa, mji ambao mbali ya kuwa makao makuu ya Umoja wa Afrika( AU) pia ndiko yalipo Makao Makuu ya Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu Uchumi wa Africa( UN-Economic  Commission for Africa).

Akihojiwa na waandishi wa habari akiwa eneo la viwanda (Hawasa Industrial Park), kuhusu mwenendo wa uchumi wa Afrika, kuhusu nchi zipi anaziona kiuchumi zikiwa kwenye nafasi ya kufanikiwa kiuchumi kama Vietnam, Singapole na Korea ya Kusini.

Aliitaja Tanzania, Ethiopia, Kenya na Nigeria.

Katika kujenga hoja yake, Largade alisisitiza hoja ya miundombinu ya uchukuzi, umeme, nguvu kazi kubwa na  yenye ubora (skilled labour force) na ukaribu wa bahari. Hili la ukaribu na bahari nadhani ni kutokana na ukweli kwamba  asilimia 90 ya  biashara ya Afrika kimataifa (export&import) inapitia usafiri wa bahari.

Hivyo, nguvu kazi yenye maarifa ni moja ya turufu muhimu katika ushindani wa biashara kimataifa na pengine hata nchini.

Tutazame kidogo hizi nchi tunazotafuta kuzifikia zimetoka wapi na zimefikaje hapo zilipo leo hii. Korea ya Kusini na Vietnam.

Nchi hizi zimekuwa mifano mikubwa kwa Bara la Afrika, kuhusu uwezekano wa kufanikisha mapinduzi ya viwanda kwa hoja kwamba mataifa haya yalikuwa na kiwango sawa kiuchumi na mataifa mengi ya Afrika ikiwamo Tanzania. Katika miaka ya 1970s pato la mwananchi wa Korea kwa mwaka lilikuwa sawa na asilimia 10 ya pato la mwananchi wa Marekani, lakini leo hii pato la mwananchi wa Korea ni asilimia 70 ya pato la mwananchi wa Marekani.

Leo Korea ya Kusini iliyokuwa na umasikini sawa na Tanzania katika miaka ya 1970s, ni miongoni mwa mataifa makubwa 20 kwa viwanda (G-20) na zaidi ni kwamba pato la raia wa Korea kwa mwaka ni dola 29,000 (IMF 2017), kiwango ambacho ni zaidi ya raia wa nchi nyingi za Ulaya kwa sasa.

Pia ni mbali mno kulinganisha na nchi zetu ambazo kwasasa pato la raia kwa mwaka ni; Kenya dola 1,700, Tanzania dola 1,400, huku Ethiopia ikiwa dola 800.

Kwa upande wa Vietnam, hadi kufikia miaka ya 1986, kabla ya mkakati wao wa kiuchumi maarufu DoiMoi, kiwango cha umasikini katika nchi hiyo kilikuwa sawa na mataifa mengi ya Afrika ikiwamo Tanzania. 

‘DoiMoi’ni neno la kikwao lenye maana ya ‘fungua mlango’ lilitumika kuelezea falsafa mpya kwa mpango wao mpya wa mwelekeo mpya wa kiuchumi mwaka 1986 kutoka uchumi hodhi wa dola (Command economy) ambapo serikali ni muhimili wa uchumi, kwenda uchumi wa soko la kijamii (social market economy), ambapo sekta binafsi inapewa nguvu ingawa kunakuwa na udhibiti wa serikali kuhakikisha upungufu ya uchumi wa soko yanadhibitiwa kwa ustawi wa jamii.

Kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia mwaka 2017, hadi kufikia miaka ya 1993 asilimia 60 ya raia wa Vietnam walikuwa chini ya mstari wa umasikini. Lakini kutokana na uongozi madhubuti na mkakati thabiti wa kiuchumi, Vietnam imefanikiwa kujenga uchumi wa viwanda na kutengeneza ajira za kutosha kwa raia wake.

Ukitazama kwa kina, hakuna sababu yoyote waliyonayo Vietnam ambayo Tanzania hakuna, au Ethiopia na Kenya wamekosa. Na ukiangalia vigezo alivyotaja Mkurugenzi wa IMF, utabaini kwamba Tanzania ipo kwenye nafasi nzuri zaidi kuliko Kenya na hata Ethiopia kama inavyosimamia kwa vitendo thabiti na mikakati yake kiuchumi.

Kwa kasi ya utekelezaji miradi ya kimkakati inayoonekana sasa, kama vile SGR, REA, n.k iwapo ingeanza miaka kumi nyuma. Nasema kwa miaka 10 nyuma kwa sababu hali ya uchumi wetu kufikia mwaka 1995 ilikuwa mbaya na ni katika awamu ya tatu uchumi ulisukwa upya na taasisi zikasimama. Vigezo vya uchumi kufikia mwaka 2005 vilikuwa vinaruhusu nchi kuanza kufanya mambo makubwa na sasa Tanzania ingekuwa mbali zaidi ya Vietnam. 

Nchi hizi tatu, Tanzania, Ethiopia na Kenya, karibu zote zina mikakati inayofanana katika kujenga uchumi ingawa zinazidiana kasi ya utekelezaji na mazingira. 

Pamoja na mikakati ya nchi hizi tatu kukaribiana kufanana, Tanzania katika maeneo yote inaonekana kuwa na nafasi zaidi kulinganisha na washindani wake hao Kenya na Ethiopia. 

Lazma Tanzania itazame ushindani huu kimkakati. Kwa mfano, Benki ya Dunia mwaka juzi imeonesha kwamba kutokana na shinikizo la kupanda kwa mishahara nchini China, ndani ya muongo mmoja kutoka mwaka juzi, mitaji itaanza kutoka China kutafuta maeneo ambayo nguvu kazi yake ina maarifa na inapatikana kwa bei ya chini. 

Kwa mujibu wa WB, inakadiriwa kuwa China itapoteza ajira zaidi ya milioni 86.

Kwa muda mrefu, China imekuwa ikiuza bidhaa nyingi za viwanda inazozalisha China huku kiasi cha malighafi kikitoka Afrika, lakini sasa mwelekeo utaanza kubadilika. China inaanza kutazama eneo la Afrika kama sehemu ya uzalishaji.

Katika sekta ya umeme, Ethiopia imeonekana kuwa mbele kwa maana ya mradi wao wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji (Hydro power), kiasi cha 6000MW, huu ni mradi mkubwa kabisa Afrika. 

Hata hivyo, Tanzania chini ya Rais Dk. Magufuli, imeamua kutekeleza mradi kama huo lakini wa 2100MW, Mradi wa Stiglers Gorge,  unaojumuisha kiasi cha umeme unaozalishwa sasa 1500MW na miradi ya KinyereziII ya 240MW itafanya Tanzania iwe kinara katika Afrika Mashariki. 

Hivyo basi, Tanzania ina nafasi nzuri zaidi kuliko washindani wake. 

Ni kweli kuna ufanisi umeongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam kwa maana ya kuongeza muda wa kazi kutoka saa nane kwa siku hadi kufikia saa 24, upanuzi wa bandari hiyo umesababisha kwasasa kupokea meli za urefu wa mita 305 itasaidia kuongeza chachu ya pato la Taifa. 

Hii ndio kusema kwamba Tanzania kwasasa ipo kwenye mstari sahihi kufaidi ushindani huo kibiashara kutokana na kuendelea kupanua na kuongeza uwezo na ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kuanza kuonesha msukumo kwenye mradi wa bandari kavu. 

Changamoto kubwa ambayo inahitaji uamuzi mgumu ni namna ya kujenga ubora wa nguvu kazi yetu. Nguvu kazi bora ni ile yenye ujuzi wa kazi na nidhamu ya kazi. Ni kweli tumeongeza vyuo vikuu kutoka vyuo vitatu hadi 46 katika kipindi cha miaka 20, lakini ukweli ni kwamba tumesahau kuwekeza kwenye vyuo vya kati, ambavyo kimsingi ndio injini katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa uzoefu wa nchi nyingi duniani zikiwamo Vietnam na Korea ya Kusini.

Ni kwa sababu hiyo, Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Viwanda limebainisha wazi kwamba asilimia 80 ya nguvu kazi yetu haina ujuzi (unskilled manpower). Pia Shirikisho la Waajiri Tanzania (Association of Tanzania Employers-ATE), limendelea kusisitiza kwamba sehemu kubwa ya wahitimu vyuo vikuu vimeongezeka kwa kasi katika miongo hii miwili. 

Ni muhimu Rais Dk. Magufuli atazame tija katika mabilioni tunayowekeza elimu ya juu kama mikopo iwapo yanafanana na tija kwenye uchumi kwa maana ya ubora wa wahitimu tunaozalisha sasa. 

Naelewa jambo hili ni nyeti hasa katika mazingira ya sasa ambayo elimu inatazamwa zaidi kwa cheti cha shahada. Siamini kama ni sahihi kuendelea kupima mafanikio ya elimu yetu kwa idadi ya wanaofaulu au kuhitimu, bali ubora wa wahitimu hao inahitaji ujasiri na uamuzi mgumu kushinikiza msingi huu lakini hakuna mbadala.

Nakumbuka kwenye kitabu cha From Third World to First World (1965-2000), Mr.  Lee Kuan Yew, ambaye ni mwasisi wa mafanikio makubwa ya nchi ya Singapore kutoka taifa fukara hadi taifa tajiri duniani, kuna mahala alizungumzia umuhimu wa kufanya uamuzi mgumu ambao ni sahihi bila kujali athari za kisiasa.

Niseme tu kwamba, kama nchi tumeangamiza elimu yetu kwa karibu miaka 30 na hivyo kuangamiza kizazi hapa katikati, ndio sababu ubora wa mijadala ya vijana wetu kwa mitandao au hata TV inapungukiwa nguvu ya hoja. 

Kuifumua na kuisuka upya ni uamuzi wenye athari kubwa kisiasa kwa sababu tayari tuna maelfu ya vyeti vinavyomilikiwa na watu lakini kichwani wana viwango duni vya elimu ukilinganisha na vyeti wanavyomiliki. 

Hili ni jipu lakini linahitaji mjadala mpana ili litumbuliwe. Jambo muhimu ni kwamba ni lazima kukabili tatizo kwa kufumua na kuweka msingi.

 Naendelea kusisitiza kwamba changamoto ni nyingi, lakini JPM yupo kwenye mstari sahihi. Mbele kuna muujiza mkubwa wa mafanikio ambayo hakuna aliyewahi kufikiri. Rais wetu wananchi tumekulewa na tupo pamoja na wewe endelea kuchapa kazi, usisikilize kelele za watu wala usijaribu kugeuza shingo yako kuangalia nyuma usije ukageuka kuwa jiwe (kama alivyowahi kusema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles