22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Juhudi zinazoendelea Makete kunusuru kaya masikini

CHRISTINA GAULUHANGANJOMBE

SERIKALI imejitahidi kufanya jitihada kadhaa kuhakikisha jamii inaondokana na umasikini uliokithiri kwa kuanzisha mifumo wezeshi inayowawezesha wananchi kuacha kubweteka na badala yake kufanya shughuli za kuwaongezea kipato.

Fursa zinazotolewa na Serikali kupitia halmashauri zake zimewezesha wanawake wengi kuacha kubweteka na kuwa mfano wa kuigwa katika familia zao.

Hali hiyo imesaidia pia kupunguza migogoro ambayo ilikuwa ikiibuka katika familia nyingi kwa sababu ya ukosefu wa kipato na wengi wao kushindwa kumudu maisha.

Wilaya ya Makete ni miongoni mwa halmashauri zinazotekeleza mpango wa kunusuru kaya maskini kwa fedha za Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mpango huo umesaidia kuzinusuru kaya maskini ambapo wengi wao walikosa uhakika wa chakula, malazi na hata elimu hali iliyosababisha uchumi wa familia nyingi kudidimia.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Makete, mkoani Njombe, Francis Namaumbo, anasema mpango wa TASAF umegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni ruzuku ya kuwalipa kaya maskini na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali kupitia mfuko huo.

“Katika mpango wa kuwalipa kaya maskini, ruzuku hiyo ni ya kusaidia kaya kwa maana ya watoto wanaotakiwa kuhudhuria kliniki na kutoa fedha taslimu ambayo siyo ya masharti,” anasema Namaumbo.

“Katika mpango wetu, Tasaf inahudumia jumla ya watoto 3,378 ambao ni wanafunzi na 387 ni wale wanaohudhuria kliniki,” anasema Namaumbo.

Anasema kwa mwaka wa fedha 2018/19 jumla ya Sh 562,301,390 zilitolewa na Serikali kupitia Tasaf ikiwa ni ruzuku ya kunusuru kaya maskini.

Namaumbo anasema katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kupitia mfuko huo, Halmashauri ya Makete imetekeleza miradi 39 yenye thamani ya Sh milioni 2.6 ambayo ipo katika vijiji mbalimbali vilivyogawanyika katika sehemu kuu tatu.

Anasema mradi huo ni pamoja na wa kujiongezea kipato, ambao wananchi wanaibua wenyewe  kulingana na hitaji la kijiji.

Anasema jumla ya miradi 15 iliibuliwa na wanajamii ambapo miradi tisa ilikuwa ni ya barabara yenye urefu wa kilometa 43.5.

Anaongeza kuwa miradi mingine mitano ni ya umwagiliaji na mmoja wa kilimo cha kuzuia mmomonyoko wa udongo.

“Mradi huo una thamani ya Sh milioni 1.1 ambapo kati ya hiyo miradi sita imekamilika na inatumika huku mingine tisa ambayo ni ya barabara ipo kwenye hatua ya utekelezaji,” anasema Namaumbo.

Miradi ya kukuza uchumi na kuongeza kipato

Miradi hii ni ya ufugaji mbuzi, ng’ombe, kilimo cha mbogamboga, ufugaji wa nyuki na kuku. Jumla ya miradi 10 yenye thamani ya Sh milioni 193.4 ni ya kukuza uchumi na kuongeza kipato na tayari imekamilika na kuwanufaisha wananchi.

Ujenzi

Miradi ya ujenzi imejikita zaidi katika sekta ya elimu na afya kutokana na hitaji la wanajamii.

Anasema jumla ya miradi 14 yenye thamani ya Sh milioni 1.2 imetekelezwa katika sehemu mbalimbali.

Namaumbo anaongeza kuwa miradi hiyo ni ya ujenzi wa madarasa,  nyumba za walimu pamoja na madaktari, zahanati na mabweni ya wanafunzi.

Anasema jumla ya miradi tisa imekamilika na inatumiwa na jamii mfano, zahanati ya Lupombwe, nyumba ya walimu wa Sekondari ya Iyoka na nyumba ya daktari.

Anasema miradi mitano ipo katika hatua za utekelezaji.

Katika kuendelea na utekelezaji wa mpango wa kunusuru kaya maskini, Tasaf iliweka mwongozo mzuri wa kuunda vikundi vya walengwa vya kuweka na kukopa.

Namaumbo anasema lengo kuu ni kuhakikisha walengwa wanajenga mazoea ya kuweka akiba na kukopa ili kujikwamua kimaisha.

Anasema halmashauri hiyo ina jumla ya vikundi 87 ambavyo vimechangishana jumla ya Sh milioni 51,5. Katika fedha hizo, kiasi cha zaidi ya Sh milioni 34 zimekopeshwa wanakikundi kwa ajili ya kufanyia kazi mbalimbali zenye manufaa.

Anasema Sh milioni 11.6 zimerejeshwa baada ya kukopwa kwa msimu huu, kwa kufuata makubaliano waliyowekeana kwenye katiba zao.

Hata hivyo, anasema wanakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na kipimo halali cha ujazo hivyo, wanaendelea kufanya mawasiliano na wadau mbalimbali wa kilimo ili kuwawezesha wakulima kunufaika na mazao yao.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Lupila, Makete, Abkasa Ngwale, anasema shule yake imeweza kunufaika na miradi ya Tasaf kwa kujengewa nyumba ya walimu, bweni la kike la kulaza wanafunzi 48, madarasa matatu yenye vyoo pamoja na nyumba za walimu kupitia miradi ya kujiongezea kipato inayosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii.

Anasema ili kuweza kuboresha zaidi shule hiyo, inahitaji kuongezewa mabweni mengine kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano kwani ina jumla ya wanafunzi 226 wanaohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wake Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Makete, Jacqueline Mroso, anasema Kijiji cha Ukange kina jumla ya  walengwa 71 ambao wamekuwa wakipata ruzuku katoka mpango wa kunusuru kaya maskini na kusaidia wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari na wale wanaohudhuria kliniki.

Anasema miradi ya kujiongezea kipato mbali na kuwanufaisha walengwa imejumuisha wananchi wa eneo zima kwa sababu imekuwa ikitatua changamoto zinazokabili jamii yote kwa ujumla na kuishirikisha jamii yote kwa pamoja ili kuweza kupata maendeleo ya pamoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles