NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
MKURUGENZI Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five Star, Ashikabbas Karim(30) na wenzake wanne, wamenusurika kwenda jela baada ya kutiwa hatiani   kufanya kazi nchini bila kibali.
Washtakiwa hao walihukumiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya washtakiwa kukiri kosa.
Mahakama iliwahukumu kulipa faini ya Sh milioni 60 au kwenda jela miaka miwili baada ya kukiri mashtaka ya kufanya kazi nchini bila kuwa na kibali cha kazi  na kuajiri raia wa kigeni.
Washtakiwa hao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho, Ashikabbas Karim(30) maarufu kama Shakirali, ambaye ni mkazi wa Upanga.
Wengine ambao ni raia wa India ni Aroygam Mocharla(38), ambaye ni mwendeshaji; Mahesh Malla Goud( 32) maarufu kama Budige, ambaye ni msimamizi wa uzalishaji; Harish Raju(35), maarufu kama Poojary ambaye ni msimamizi na Kiran Subbarayudu(30) maarufu kama Koneti ambaye ni fundi, wote wakazi wa Vingunguti.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita, yakiwamo ya kuajiri raia wa kigeni ambao hawana vibali vya kazi.
Hakimu Simba alisema mahakama inawatia hatiani washtakiwa kama walivyoshtakiwa na   wanatakiwa kila mshtakiwa kulipa faini ya Sh milioni 10 kwa kila kosa au kwenda jela miaka miwili iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.
Alisema mshtakiwa wa kwanza, Karimu, anakabiliwa na mashtaka mawili ambayo ni kuajiri raia wa kigeni bila kuwa na kibali cha kazi na shtaka la pili ni kuzuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao.
“Mshtakiwa wa kwanza atatakiwa kulipa faini ya Sh milioni 10 kwa kila kosa au kwenda jela miaka minne, mshtakiwa wa pili hadi wa tano, kila mmoja atalipa faini ya Sh milioni 10 au jela miaka miwili,”alisema.
Alipotakiwa kuwazungumzia washtakiwa, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Arnold Peter akishirikiana na Charles Boaz, alisema hawana kumbukumbu ya makosa ya nyuma hivyo mahakama itoe adhabu kwa mujibu wa sheria.
Wakili wa Utetezi, David Ndosi akishirikiana na Benedict Alex, aliomba mahakama iwapunguzie adhabu kwa sababu  ni kosa lao la kwanza na pia wamekiri makosa yao na hawakusumbua mahakama.
Katika hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo Julai 12, 2018 katika Kiwanda cha Uchapishaji cha Five Star kilichopo eneo la Vingunguti, Wilaya ya Ilala.
Katika shtaka la kwanza ambalo linamkabili mshtakiwa wa kwanza, inadaiwa kuwa Julai 12, 2018 katika kiwanda hicho, Karim aliwaajiri wafanyakazi wake ambao ni Mocharla, Goud, Raju na Subbarayudu, katika kiwanda chake bila kuwa na kibali cha kazi.
Katika shtaka la pili ambalo linamkabili mshtakiwa wa kwanza , inadaiwa   siku hiyo ya tukio katika kiwanda hicho, Karim alizuia maofisa wa Serikali kutekeleza majukumu yao ya kazi kwa kuwaficha ndani wafanyakazi wake wanne,   Mocharia, Goud, Poojary na Kumar katika ghala iliyopo kiwandani hapo.
Katika shtaka la tatu hadi la sita  ambalo linawakabili mshtakiwa wa pili hadi wa tano, inadaiwa kuwa siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakifanya kazi kiwandani hapo bila kuwa na kibali cha kazi.