Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga, Amis Tambwe na nahodha wa Simba, Jonas Mkude, wameanza kuwatikisa vigogo wa klabu hizo baada ya kusisitiza kwamba hawawezi kuongeza mkataba bila kupewa dau nono la usajili.
Tambwe, ambaye amekipiga Yanga tangu msimu wa 2014/15, ameueleza uongozi wa klabu hiyo kuwa, hataweza kuongeza mkataba mpya kama utashindwa kumshawishi kwa kumuongezea dau mkataba wake utakapokwisha Mei, mwakani.
Uongozi wa Yanga una kila dalili ya kutaka kumuongezea mkataba straika huyo kutoka Burundi, baada ya kuridhishwa na kiwango alichokionesha msimu uliopita na katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Tambwe alisema hajafanya mazungumzo yoyote na Yanga kuhusu kuongeza mkataba, lakini yapo mambo yanayoweza kumshawishi, ikiwamo kuongezewa dau la usajili ili aendelee kukipiga kwa Wanajangwani hao.
Alisema anafikiria kucheza soka nje ya Tanzania na hilo linaweza kutokea kama Yanga watashindwa kuongeza dau katika mkataba wake mpya.
“Kuna klabu zimeonesha nia ya kuhitaji saini yangu, lakini siwezi kuziweka hadharani kwa sasa hadi nitakapomalizana na klabu yangu,” alisema Tambwe.
Kwa upande wake Mkude, ambaye alinufaika na Sh milioni 60 katika mkataba wake unaomalizika, ameutaka uongozi wa Simba kuongeza dau na kumlipa Sh milioni 80 ili akubali kusaini.
Chanzo cha habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana, kilidai kuwa makocha wamesisitiza kwamba kama ataendelea kushikilia msimamo wake wataachana naye, kwani tayari wamepata mbadala wake.
Licha ya kiungo huyo kuwa na umuhimu ndani ya kikosi cha Simba, makocha wamepanga kumtumia Mzamiru Yassin, aliyetokea Mtibwa Sugar, kama mbadala wa Mkude.
Wekundu hao wa Msimbazi tayari wamemalizana na beki wao wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, ambaye pia mkataba wake ulikuwa unaelekea ukingoni kwa kumuongezea mkataba wa miaka miwili, huku wakiendelea kuwashawishi Mkude na Ibrahim Ajib.