29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MKOA WA MARA WAPIGA HATUA UZAZI WA MPANGO

Na Mwandishi Wetu

MKOA wa Mara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa  kupiga hatua kubwa kwenye matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Imeelezwa kati ya mwaka 2010 na 2015, mkoa huo umefanikiwa kuongeza matumizi ya njia hizo kutoka asilimia 11 hadi asilimia 29 katika kipindi hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Dar es Salaam, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk. Nila Jackson alisema hatua hiyo imetokana na uongozi kujitolea na kuungwa mkono na wananchi ambao wametambua umuhimu wa uzazi wa mpango katika mipango ya maendeleo.

Dk. Jackson, alitoa kauli hiyo baada ya kushiriki  mkutano wa kubadilishana mawazo na wadau wa uzazi wa mpango.

Alisema mafanikio ya mkoa huo, pia yametokana na kuendesha mikutano ya kila mwezi ya wadau husika kuangalia takwimu za matumizi ya huduma za uzazi wa mpango, kuzungumzia changamoto zilizopo na kuweka mikakati ili kuongeza kasi ya utekelezaji ya huduma hasa kwa kutoa taarifa na elimu juu ya njia sahihi.

Alisema kwa kushirikiana na wadau wa afya, kwa mfano, Serikali ya mkoa ilianzisha kampeni maalumu ya kutoa elimu ili kuhamasisha watu kutumia uzazi wa mpango na kuinua kiwango kidogo kilichoiweka nyuma Mara miaka kadhaa iliyopita.

Alisema wamekuwa wakiwashirikisha kikamilifu wazee wa mila  kuzungumzia na kutilia mkazo uzazi wa mpango.

“Mila na desturi katika mkoa huu, zimekuwa sehemu ya changamoto zilizokuwa zikikwamisha harakati hizi, hivi sasa viongozi wa kimila wamekuwa chachu ya mafanikio yetu,”alisema Jackson.

Alisema japo kwa kasi ndogo, Tanzania imefanikiwa kuongeza matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kutoka asilimia 27 mwaka 2010 hadi asilimia 32 mwaka 2015.

Alisema imejiweka lengo la kufikia asilimia 45 katika matumizi ya uzazi wa mpango, ifikapo mwaka 2020 katika jitihada za upunguza vifo vya akina mama ambavyo vimepanda hadi 556 katika kila vizazi hai 100,000 kutoka vifo 454/100,000 mwaka 2010.

Kwa upande wake, James Mlali wa Kituo cha Mawasiliano na Maendeleo ya Jamii (TCDC),  mshirika mmoja wapo wa mradi wa Advance Family Planning, alisema uwekezaji zaidi kwenye uzazi wa mpango kutoka Serikali kuu unahitajika ili kuongeza kasi ya matumizi na kufikia lengo la Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles