27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

PROF. MUKANDALA: VIJANA MSISUKUMWE NA MAWIMBI

Na Mwandishi Wetu

-DAR ES SALAAM

MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala, amewataka vijana wanaohitimu kidato cha sita nchini wawe makini na wasikubali kusombwa na mawimbi ya dunia.

Kauli hiyo aliitoa juzi, wakati akizungumza na wahitimu 237 wa kidato cha sita wa Shule ya Sekondari ya St. Joseph Cathedral katika mahafali ya sita ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo, jijini Dar es Salaam.

Kwa hatua mliyofikia kila mmoja anapaswa atafakari kwa kina wito wake kimaisha. Kuweni makini msisukumwe na mawimbi ya dunia na kujikuta mmepoteza ndoto zenu.

“Kuhitimu kidato cha sita si jambo dogo. Ni hatua ya kuwaongoza kujiandaa na utu uzima ikiwemo kujiunga na elimu ya vyuo vya juu na kuingia kwenye ndoa.

“Ni muda wa kutathmini yale uliyopitia na kutafakari maisha yako ya baadaye. Ni fursa ya kutoa shukrani kwa Mungu, kwa wazazi na walimu ambao walifanya kazi kwa umakini na kujitoa ili mfikie hatua nzuri mliyopo sasa,” alisema Prof. Mukandala.

Alisema kuanzia sasa kila mmoja wao anapaswa kujiamini, kujituma zaidi na kujiona kuwa ana wajibu wa kujiletea maendeleo binafsi.

“Mnapaswa kuepuka mwenendo wa kujiona mnyonge, au mtu asiyeweza kutimiza ndoto zake. Jenga tabia ya kuwa makini na maisha yako, jali mazingira yako na maendeleo yako,” alisema.

Aliwataka wahakikishe wanachukua hatua mahsusi na kupata taarifa sahihi kuhusu taaluma wanazozitaka.

Aliwataka wawe waadilifu na wenye heshima kwa watu wote lakini pia akawaasa juu ya maisha ya kutaka kupata fedha kwa haraka na kujilimbikizia mali.

“Epukeni rushwa na ufisadi. Mnatakiwa kujua kuwa utu, maendeleo na maisha bora havipatikani kwa fedha ingawa nayo ni muhimu katika maisha. Msitegemee kuishi kwa kuzingatia mambo makubwa yanayopimika kwa fedha,” alisema.

“Msikimbilie kuwa na magari mengi bila kujua nani atayatumia au kujenga nyumba kubwa bila kujua nani atahitaji nafasi hiyo kubwa.

“Unanunua simu mbili au tatu bila kufikia athari zake kwa afya na mahusiano yako. Kabla hujachukua hatua ni lazima ujiulize, je unakihitaji kitu hicho? Kuweni makini na matumizi ya fedha badala ya kulimbikiza vitu vya anasa,” alisema.

Aliwataka wazazi waendelee kuwalea vema vijana hao kwa sababu bado wanahitaji usimamizi wa wazazi kwa kila hatua wanayosonga mbele.

“Tuendelee kuwaunga mkono watoto wetu kwa sababu jukumu letu kama wazazi bado liko palepale,” alisema.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya St. Joseph Cathedral, Sista Theodora Faustine alisema anaamini wahitimu wote watakuwa na sifa za kujiunga na vyuo vikuu mwaka huu.

“Tumekuwa tukipata wanafunzi bora kitaifa mara kwa mara na mwaka jana tulipata wanafunzi bora kutoka michepuo ya PCB na ECA,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles