Na ESTHER MNYIKA
-DAR ES SALAAM
MKEMIA Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele amesema sampuli za watu wanaotumia dawa za kulevya zimeongezeka kwa kipindi cha miezi miwili hadi kufikia 1,000 kutoka 644 ambapo pia wanatarajia kupokea kesi za aina hiyo 3,600 hadi kufikia Desemba mwaka huu.
Aidha, kutokana na wingi wa kesi hizo hivi sasa inawalazimu kwenda Kwa Mpiga Chapa wa Serikali kuchukua karatasi za siri ili kuepuka kuvuja kwa majibu hayo na wafanyakazi kulipwa malipo ya ziada kutokana na kufanya kazi kwa saa 18.
Takwimu hizo za Mkemia Mkuu zimekuja muda mfupi baada ya hivi karibuni Mkuu wa Dar es Salaam, Paul Makonda kutaja watu wanaotuhumiwa kujihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya ambapo katika orodha hiyo aliwataja baadhi ya wasanii, wanasiasa, viongozi wa dini na wafanyabiashara.
Profesa Manyele amesema hayo leo wakati akitoa taarifa ya serikali kuhusu ununuzi wa mtambo wa kisasa wa kupima sampuli tofauti unaoitwa 'energy Dispersive X-Ray Flourescence SPectrometer' (EDXRF) ambao umegharimu Sh milioni 101.7.
“Kutokana ongezeko la kupima sampuli za dawa za kulevya tunalazimika kusitisha kupima sampuli nyingine kwa lengo la kuwahisha majibu ya watuhumiwa wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama ili hatua za kisheria zichukuliwe, hivyo kutokana na ongezeko la kesi hizo, tumeanzisha kitengo maalumu kwa ajili ya kupokea kesi za dawa za kulevya tu ili kurahisha majibu ya kesi hizo kupatikana kwa wakati na kufanyia matengenezo mitambo husika,” amesema Profesa Manyele.