30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MKE WA KINGUNGE AFARIKI DUNIA, MWENYEWE ALAZWA ICU

Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam


MKE wa mwanasiasa mkongwe nchini, Peras Kingunge Ngombale Mwiru, amefariki dunia jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, huku hali ya afya ya mumewe ikiwa si nzuri.

Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, mtoto mkubwa wa Kingunge, Kinje, ambaye muda mwingi alikuwa akilia, alikiri mama yake kufariki dunia, huku baba yake akilazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali hiyo.

Kingunge (88) amelazwa Muhimbili karibu wiki mbili sasa baada ya kung’atwa na mbwa sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Mama amefariki hata baba (mzee Ngombale) hajui juu ya jambo hili kwa sababu naye ni mgonjwa ndiyo kwanza ametolewa theatre (chumba cha upasuaji) anaumwa… aling’atwa na mbwa nyumbani tutamueleza atakapoamka,” alisema.

Kinje alisema kuwa mama yake alianza kupatiwa matibabu hospitalini hapo kutokana na tatizo la kupooza mwili tangu mwishoni mwa mwaka jana.

“Mama alianza kupooza tangu mwaka jana, tukamhamishia Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi, lakini Mungu amempenda zaidi,” alisema Kinje.

Alipoulizwa baba yake amefanyiwa upasuaji wa nini, Kinje alishindwa kuzungumza kutokana na muda mwingi kulia.

Naye Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, John Steven, alithibitisha kifo cha Peras na kusema kuwa alilazwa hospitalini hapo tangu Oktoba 3, mwaka jana.

“Kweli mama Kingunge amefariki mchana wa leo (jana), wakati akiendelea kupatiwa matatibu hapa,” alisema.

AFYA YA KINGUNGE

Mmoja wa wana familia hiyo, Toni Kingunge, aliiambia MTANZANIA kuwa hadi jana machana, Kingunge alikuwa amelazwa ICU, akisubiri kufanyiwa upasuaji.

“Mzee amelazwa ICU kutokana na matatizo yanayomkabili, si kwamba ana hali mbaya, lakini madaktari wamempumzisha huko kwa ajili ya uangalizi… ana matatizo kwa sababu alishambuliwa na mbwa akiwa nyumbani kwake,” alisema Toni.

Alisema Kingunge alishambuliwa na mbwa karibu wiki mbili na nusu zilizopita nyumbani kwake Victoria, Dar es Salaam nyakati za asubuhi alipokuwa akitoka kwa ajili ya kufanya mazoezi.

“Baba alishambuliwa na mbwa karibu maeneo manane tofauti mwilini mwake, sasa hali hiyo imemletea matatizo ambayo jopo la madaktari wanahangika kumtibu, licha ya kupata tiba ya awali ya kuzuia wadudu au sumu hatarishi.

“Hawa mbwa kwa kawaida hufungiwa ndani ya banda pale nyumbani, siku hiyo inaonekana mzee wakati anatoka walikuwa hawajafungiwa, wakaanza kumshambulia ovyo, tukajitahidi tukamwahisha hospitali kupata tiba za awali,”alisema Toni.

Alisema hadi jana, Kingunge alikuwa na tatizo jingine la kuvimba miguu jambo ambalo hawajajua limesababishwa na nini.

“Mzee anajitambua mpaka muda huu, lakini ana tatizo la kuvimba miguu na vile vidonda alivyong’atwa na mbwa vinaendelea vizuri, tunaamini akiwa ICU atapata matibabu zaidi… mie niko nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya msiba wa mama, nitakupa mawasiliano ya Kinje ambayo yuko na mzee Muhimbili akueleze zaidi,” alisema Toni.

Kuhusu msiba wa mama yao, alisema taratibu nyingine zinaendelea kufanyika na ratiba kamili itatolewa wakati wowote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles