BADI MCHOMOLO
UKIWATAJA washambuliaji bora katika Ligi ya nchini Italia, Serie A, hauwezi kuliacha jina la mshambuliaji wa timu ya Inter Milan, Mauro Icardi.
Nyota huyo katika misimu kadhaa iliopita alikuwa anaingia kwenye orodha ya washambuliaji bora huku wakati mwingine akiwa kinara hadi mwisho wa msimu huu.
Mambo yamekuwa magumu msimu huu ambapo hadi sasa ana jumla ya mabao tisa baada ya kucheza michezo 20, wakati huo Fabio Quagliarella ambaye anakipiga katika klabu ya Sampdoria akiwa na mabao 21 baada ya kucheza michezo 27.
Nyuma ya mafanikio yake yupo mke wake Wanda Nara, ambaye pia amekuwa msimamizi wake wa mambo ya soka kwa jina lingine ni wakala.
Wanda ni wakala wa mume wake, amekuwa akisimamia uhamisho wa mchezaji huyo na manufaa yoyote kutokana na mikataba yake ya soka.
Mbali ya kuwa wakala wake, lakini amekuwa chanzo cha migogoro mbalimbali ambayo Icardi anakutana nayo kwa kipindi cha misimu kadhaa.
Migogoro hiyo inachangia kushusha kiwango chake uwanjani na kumfanya mchezaji huyo thamani yake ishuke.
Wanda alikuwa mtangazaji wa vipindi vya runinga na mwanamitindo maarufu nchini Argentina, alifanikiwa kufunga ndoa na Icardi mwaka 2014 na tayari wamefanikiwa kupata watoto wawili katika ndoa yao.
Hiyo haikuwa ndoa ya kwanza kwa Wanda, aliwahi kufunga ndoa na mchezaji wa zamani wa Argentina, Maxi Lopez, ambaye aliwahi kucheza katika klabu mbalimbali kama vile Barcelona, River Plate, Chievo, Udinese, Torino na zingine.
Wawili hao walifunga ndoa tangu mwaka 2008 kabla ya kuja kuachana 2013, huku miezi michache baadae akaja kufunga ndoa na rafiki wa mchezaji huyo Icardi mwaka 2014.
Hiyo ilikuwa habari kubwa kwenye vyombo vya habari, huku Icardi akidaiwa kumgeuka rafiki yake Lopez na kumuoa aliyekuwa mke wake wakati wawili hao walikuwa marafiki wakubwa ndani ya kikosi cha Sampdoria kuanzia mwaka 2011 hadi 2012.
Wachezaji wakaanza kumtenga Icardi kwa kitendo cha usaliti alichokifanya, lakini wala hakujali, mchezaji huyo aliendelea na maisha na mrembo huyo na kuja kumfanya wakala wake mwaka 2016 baada ya kumfukuza kazi aliyekuwa wakala wake.
Tangu hapo Icardi na Lopez hawana urafiki tena, wamewahi kukutana zaidi ya mara mbili wakiziwakilisha timu zao kwenye michuano mbalimbali ikiwa pamoja na Ligi Kuu, lakini Lopez hataki salamu na mchezaji huyo wala kushikana mikono kwa kuwa bado anaumia kwa kitendo alichokifanya cha kumuoa aliyekuwa mke wake ikiwa ni miezi minne tangu waachane.
Kwa sasa Wanda amekuwa akiyaendesha maisha ya mchezaji huyo kwa asilimia kubwa na kumsababishia kugombana na familia yake pamoja na klabu yake ya Inter Milan.
Icardi amevuliwa unahodha wa kuiongoza Inter Milan kutokana na wakala wake Wanda kushindwa kufikia makubaliano juu ya mchezaji huyo kuongezewa mkataba mpya.
Inasemekana kwamba Wanda tayari amefanya mazungumzo na uongozi wa Real Madrid kwa ajili ya kuona uwezekano wa kuhamia timu hiyo, hivyo amegoma kufanya mazungumzo na Inter Milan juu ya mkataba mpya.
Hata hivyo, Icardi alionekana kuwa jeuri na kugoma kufanya mazoezi ya pamoja na klabu yake kwa wiki sita kabla ya mwishoni mwa wiki iliopita kuungana na timu.
Kwa upande mwingine, familia ya Icardi imekuja juu kutokana na mwenendo wa mchezaji huyo katika soka na kudai yote hayo yanasababishwa na wakala wake ambaye pia ni mke wake Wanda.
Dada wa mchezaji huyo Ivana, amedai sababu ya Inter Milan kumtoa mchezaji katika nafasi ya unahodha ni mwenendo mbaya wa mke wake Wanda na kumfanya mchezaji huyo kushuka kiwango pamoja na kugombana na familia.
Ivana amedai, Wanda anasababisha maisha ya kaka yake yayumbe na kumfanya mchezaji huyo kuwa na kiburi ambacho kinamsababishia kugombana na familia pamoja na viongozi wa timu.
Icardi hataki kusikiliza maneno kutoka kwa familia yake hasa katika kumzungumzia juu ya mama wa watoto wake huyo, huku akiamini kuwa anafanya kazi kubwa ya kuhakikisha soka lake linazidi kufika mbali.
Mchezaji huyo anahusishwa kuwindwa na klabu mbalimbali Ulaya ikiwa pamoja na mabingwa wa soka Ulaya, Real Madrid hasa baada ya kumalizika kwa msimu huu, lakini kuachwa benchi kwenye kikosi chake kunaweza kumpunguzia makali yake uwanjani na kumfanya thamani yake ishuke.