Derick Milton Na Grace Shitundu-SIMIYU
RAIS mstaafu Benjamin Mkapa, amesononeshwa na kuibuka mara kwa mara kwa migogoro ya ardhi inayohusisha makundi ya wakulima na wafugaji nchini.
Amewataka watendaji wa Serikali kuhakikisha wanakamilisha mpango wa matumizi bora ya ardhi, ambao ndio utakuwa mwarobaini wa kuikomesha.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Bariadi mkoani hapa wakati wa kilele cha Sikukuu ya Wakulima, maarufu Nanenane.
Alisema ili kuepuka migogoro inayotokea kati ya wakulima na wafugaji, ni kila mmoja kuwa na mahali pa kufanyia shughuli zake.
“Hivyo basi, kwa watendaji wote wa Serikali ni lazima mkamilishe kwa wakati mpango wa matumizi bora ya ardhi haraka iwezekanavyo na kwa wakati ili wakulima, wafugaji na wavuvi wafanye shughuli zao bila ya kugombana,” alisema.
Mkapa alitoa rai kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kuhakikisha wanaisaidia kutatua migogoro ya ardhi ili wakulima na wafugaji wapate sehemu ya kufanya kazi.
“Natoa rai kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji ili mfugaji apate mahali pa kufuga na kupata maji ya kunyweshea mifugo yake na wakati huohuo mkulima naye apate eneo ambalo anaweza kulima bila ya kuingiliwa na mfugaji,” alisema Mkapa.
Mkapa ambaye alimwakilisha Rais Dk. John Magufuli kwenye kilele hicho, alisema kwa sasa eneo lililotengwa na Serikali kwa ufugaji ni hekta milioni 2.5 katika vijijini 741 kwa nchi nzima.
Alisema Serikali kupitia halmashauri zote nchini kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, tayari wameshaandaa mpango ikiwa ni mkakati wa kuondoa migogoro hiyo.
Licha ya hali hiyo, alisema Serikali inaendelea kuboresha sekta ya kilimo kwa mazao mbalimbali na kwamba itahakikisha inaongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 100,000 hadi milioni moja kufikia mwaka 2020.
RUKSA KUUZA MAZAO NJE
Mkapa aliwatangazia wakulima na wafanyabiashara kwamba kuanzia sasa Serikali imeruhusu kuuza mazao nje ya nchi.
Alisema uuzaji huo ni lazima ufuate sheria, kanuni na taratibu za uuzaji wa mazao hayo nje.
Licha ya Serikali kuwaruhusu wananchi kuuza nje ya nchi, Mkapa aliwataka kuhakikisha wanaweka akiba ya chakula kwa kutouza chote.
“Kwa sasa Serikali imeondoa zuio la kuuza mazao nje ya nchi, hivyo ni ruksa kuuza mazao nje ya nchi, lakini lazima mfuate sheria, taratibu na kanuni za kuuza mazao hayo. Na niwatake wananchi kutouza chakula chote, wekeni akiba ya chakula,” alisema Mkapa.
Awali akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, alisema alitangaza maonyesho hayo kufanywa kitaifa mara tatu mfululizo katika Kanda ya Ziwa Mashariki ambayo inabeba mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara.
Alisema kutokana na kanda ilivyoandaa na maonesho hayo, ni lazima ijipange ili mwaka ujao yawe ya kimataifa huku akiutaka Mkoa wa Simiyu kuwa wa mfano.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, alisema vijana na makundi mbalimbali wajitokeze kutumia uwanja wa maonyesho ya Nanenane kwa kuendeleza kilimo biashara.
“Uwanja huu utakuwa una maonyesho ya kilimo, biashara kila baada ya miezi mitatu, hivyo wajitokeze ili kuufanya kuwa wa kijani kwa mazao,” alisema.
- BASHIRU AWASHUKIA MA-RC
Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally, amewashukia wakuu wa mikoa wasiokuwa na ushirikiano mzuri na uongozi wa chama hicho na kuwataka kujirekebisha mara moja.
Alitoa kauli hiyo wakati akitoa salamu za chama katika maadhimisho hayo ya Nanenane.
Alisema kuna mikoa inaongoza kwa migogoro kati ya wakuu wa mikoa na watendaji wa CCM ambao ndio watekelezaji wa ilani ya chama.
Aliitaja mikoa inayoongoza kwa migogoro kuwa ni Mara, Arusha, Mbeya na Dar es Salaam huku Simiyu, Dodoma, Singida na Pwani akiitaja kuwa vinara wa ushirikiano.
“Tumeumizwa sana na makundi ndani ya chama na Serikali kwa muda mrefu, hivyo mikoa inayoongoza kwa kuwa na ushirikiano mzuri ninaipongeza. Hata hivyo wasibweteke, lakini kwa wale ambao wanaogoza kwa migogoro nawataka wajirekebishe mara moja,” alisema Dk. Bashiru.