31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

ZITTO AZUIWA KUHUTUBIA TARIME

ANDREW MSECHU Na ASHA BANI


KIONGOZI wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe jana alijikuta akikwama kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Turwa wilayani Tarime kupitia Chadema, Charles Mnanka,  baada ya Jeshi la Polisi kumzuia kuhutubia kwa kuusambaratisha mkutano kwa mabomu ya machozi.

Zitto ambaye alialikwa kwenye mkutano huo pamoja na viongozi wa Chadema wakiwa kwenye eneo la tukio, alifika Mkuu wa Polisi Wilaya ya Tarime (OCD) na kuwamuru viongozi na wananchi   kutawanyika kwa sababu jeshi hilo halikuwa na taarifa ya kuwapo kwao.

Akizungumza baada ya kutawanywa   mkutano huo na mabomu ya machozi, Zitto alilalamikia hatua ya  Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya akisema hatua hiyo ni ukiukwaji wa haki na sheria za uchaguzi.

Alisema katika tukio hilo, zaidi ya watu 22 akiwamo Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko na mwandishi wa habari, wa Gazeti la Tanzania Daima, Sitta Tuma, walikamatwa na kushikiliwa katika Kituo cha Polisi.

Zitto ambaye chama chake kimetangaza kuungana na Chadema katika uchaguzi wa marudio wa ubunge na udiwani unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu, alisema hatua hiyo ya polisi kuvamia na kutawanya mkutano huo bila ya taarifa rasmi ni ukiukaji wa Katiba na taratibu za uchaguzi.

“Mkutano wa hadhara wa kampeni wa sheria kwa mujibu wa Katiba na kwa mujibu wa sheria za uchaguzi, upo kwenye ratiba ya kampeni za udiwani za mgombea wa Chadema kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi,” alisema.

Alisema alifika kuhutubia mkutano huo kwa mwaliko wa viongozi wa Chadema Mkoa wa Mara kupitia Katibu Wilaya na Mbunge Matiko na akiwa pamoja na viongozi wa ACT alifika kutimiza wajibu wake akitarajia kushirikiana na wenyeji wake.

Akisimulia namna ilivyotokea, Zitto alisema baada ya kufika Tarime, alielezwa na viongozi wa Chadema mkoa kuwa walipata taarifa za ghafla walizopewa kwa mdomo kutoka polisi kuwa mikutano yote ya Chadema imezuiliwa kuanzia leo (jana Agosti 8) hadi Jumamosi Agosti 11 kwa sababu ambazo polisi wenyewe wanazijua.

Alisema kwa kuwa huo si utaratibu, waliamua kufanya mkutano kwa kuwa ulikuwa umeshaandaliwa lakini polisi walivamia na kuuzingira.

Alisema waliwazuia  kuendelea na mkutano huo wazungumzaji waliokuwa wameandaliwa ambao ni Zitto mweyewe, Mbunge wa Geita (Viti Maalumu Chadema) Peneza na Matiko (Tarime Mjini Chadema).

Zitto alilaani kitendo hicho alichodai ni cha uvunjifu wa sheria kwa kuwa utaratibu uko wazi kwamba iwapo kuna tatizo linalolalamikiwa utaratibu unaelekeza msimamizi wa uchaguzi.

Alisema msimamizi wa uchaguzi  anatakiwa kuwaita kwa maandishi viongozi wa kata/jimbo wanaohusika kwenye vikao vya kamati ya maadili, jambo ambalo halikufanyika, bali walichukua hatua ya kutumia polisi kuvuruga mkutano huo.

“Kinachoonekana ni kwamba CCM wameshashindwa katika kata hii, hivyo wameamua kufanya makusudi kuvuruga uchaguzi kwa kuendesha vitisho kwa kutumia vyombo vya dola  kuwavunja moyo wananchi kushiriki uchaguzi, au kwa kufanya uchaguzi usiwepo au kuwavuruga wananchi wasijitokeze kupiga kura   wamtangaze wanayemtaka,” alisema.

Alisema hata baada ya kukamatwa   watu 22 waliokuwa kwenye mkutano huo, yeye na mbunge wa Viti Maalumu, Upendo Peneza, walifika kituo cha polisi wanakoshikiliwa  kujua kinachoendelea na hali ya mbunge Matiko, katibu wake na mwandishi anayeshikiliwa, lakini walifukuzwa kituoni hapo.

Alisema hadi jana jioni walikuwa wakiendelea kuwasiliana na wanasheria na viongozi wengine  kujua hatua wanazoweza kuchukua kutokana na tukio hilo.

Zitto aliwataka wananchi wa Tarime watulie wakati wakiendelea kufuatilia na kuwasiliana na polisi makao makuu  kuhakikisha  amani haivurugiki na wananchi wanapewa uhuru na fursa ya kuchagua mgombea wanayemtaka na si anayetaka kuwekwa na CCM.

Hata hivyo, muda mfupi baada ya kukamatwa, Sitta ambaye ni mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima aliweza  kuandika ujumbe mfupi uliokuwa ukisomeka “Habari kaka Edwin. nipo Tarime nimekamatwa na polisi nikiwa natekeleza majukumu yangu ya uandishi wa habari.

“Nimekamatwa baada ya polisi kuutawanya mkutano wa Chadema  wa kampeni kata ya Turwa Tarime kisha baadaye wakaanza kufyatua mabomu ya machozi. nikiwa napiga picha tukio la Mbunge wa Tarime mjini Ester Matiko ndiyo polisi wakanikimbilia na kunikamata”.

Mwandishi na Mtetezi wa Haki za Binadamu,  Edwin Soko, aliandika barua kwa Jeshi la Polisi kumtambua  Tumma ni mwandishi na alikuwa katika eneo hilo akitekeleza majukumu yake .

“Tuna imani Jeshi la Polisi lina weledi wa kutambua makosa ya jinai na taratibu za kushughulikia makosa ya jinai kadri sheria zinavyoelekeza.

“Tuna imani IGP na RPC wa Tarime/Rorya watalishughulikia suala hili na mwandishi Tumma ataachiwa  aendelee na majukumu yake ya uandishi wa habari na kulinda uhusiano baina ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari,’’ ilieleza sehemu ya ujmbe huo kwenda Jeshi la Polisi Tarime

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalimu ya Tarime/Rorya,  Henry Mwaibambe, alisema Jeshi la Polisi lilipata nakala ya barua kutoka NEC kuzuia mkutano huo lakini Chadema walilamikia hatua hiyo kwa kutaka wapewe notisi ya saa 48.

“Tuliamua kutumia nguvu kuwatawanya baada ya waliokuwa kwenye mkutano kuamua kuandamana kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi suala ambalo ni kinyume cha utaratibu. Na tumewakamata watu 17 ambao sasa tunaendelea na mahojiano nao baada ya hapo tutatoa utaratibu wa dhamana,” alisema Kamanda Mwaibambe

Alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa mwandishi wa Tanzania Daima, Sitta Tuma, alisema alikamatwa kwa kuwa alikuwa mstari wa mbele wakati wenzake walikuwa pembeni.

“Ushahidi wa maelezo yake ndiyo utakaomfanya atoke katika kundi hilo au vinginevyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles