28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa aponda uteuzi wa viongozi

Elias Msuya na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
RAIS mstaafu, Benjamin Mkapa, amekosoa uteuzi wa viongozi wa umma nchini akisema sera ya utumishi wa umma inayojali utaalamu haifuatwi.
Ametoa kauli hiyo wiki chache baada ya kuzuka mjadala wa uteuzi wa wakuu wa wilaya uliofanywa na Rais Jakaya Kikwete, huku ikielezwa haukuzingatia weledi, maadili na uzoefu kwa walioteuliwa.
Akizungumza katika siku ya pili ya uzinduzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam jana, Mkapa aliyekuwa mtoa mada, alisema kutojali taaluma ni kati ya mambo yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Jambo moja ninalodhani limeturudisha nyuma katika maendeleo na mnisamehe kwa kusema hili, ni sera ya utumishi wa umma.
“Tunajua kanuni za kuhamisha mtu kutoka sehemu moja kwenda nyingine, iwe ni kwa utawala wa jumla au kwenye nafasi za utaalamu. Hapa ndipo tulipopotea.
“Mzee Msuya (Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya) atakuwa amewaambia, wakati ule hata ukimaliza chuo kikuu, bado utapewa nafasi kama ofisa maendeleo ya jamii na utapitia mafunzo ili kupanda vyeo.
“Utakuwa ofisa mwandamizi au hata kamishna, lakini leo unaweza ukawa mtu yeyote na ukapangwa popote,” alisema Mkapa huku akishangiliwa na washiriki wa kongamano hilo.
Akijibu swali kama nchi za Afrika zinaweza kuendelea huku zikitegemea misaada ya wahisani, Mkapa alisema nchi zilizoendelea zina mkakati wa kuhakikisha nchi zinazoendelea haziendelei.
“Ni kweli, tunaambiwa kwamba tunashindwa kushindana na uchumi wa nchi zilizoendelea na hii ni kwa sababu wana mkakati wa kuhakikisha hatuwafikii, wanataka unyonyaji wao uendelee,” alisema Mkapa.
Akizungumzia umasikini unaolikabili Bara la Afrika, alisema jukumu la Serikali ni kuwajibika katika kuondoa umasikini wa kipato, chakula, elimu, afya, watu kushindwa kumiliki mali na kutoshiriki katika siasa.
Alisema kuwajibika kwa Serikali ni muhimu katika kujenga mfumo wa uchumi na umilikaji wa rasilimali kwa wananchi.
“Kwa sababu wananchi wengi ni wakulima wadogo na wafugaji, kigezo kikubwa cha maendeleo ni kuwamilikisha ardhi,” alisisitiza Mkapa.
Kuhusu dira ya taifa, alisema Serikali inatakiwa kuitofautisha na mipango ya maendeleo ya kila mara ili ieleweke.
Awali, akitoa mada ya kurejea kwa maendeleo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi na Mipango ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa na Afrika, Profesa Adebayo Olukoshi, alisema jukumu la Serikali duniani kote ni kupambana na umasikini wa wananchi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles