Na Fredy Azzah, Dodoma
Waziri Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, amesema kiasi kikubwa cha mkaa unaotoka nchini unaenda kutumiwa kwenye mataifa mengine ikiwa ni pamoja na Somalia na Uarabuni.
Makamba alisema hayo jana wakati akihitimisha hoja za kupitisha Azimio la Bunge la kuridhia Makubaliano ya Paris chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi, Makambo.
Amesema mkaa huo hutoka nchini kupitia bandari za Bagamoyo, Mbweni na nyingine za Pwani kwenda Pemba na baadaye Shimoni Mombasa.
“Ukiangalia mkaa mwingi unaoenda Pemba ni magunia ambao hauendani na watu wa Pemba, ukifika Pemba wanapeleka Shimoni na baadaye Somalia unaenda kuwa mtaji kwa Al shabaab, mwingine unaenda uarabuni kuchoma kondoo kwa sababu waarabu wanapenda mkaa mzuri wa kuchoma kondoo.
“Kwa hiyo utaona mkaa unakatwa huku unaenda kunufaisha watu wengine huko,” amesema Makamba.