NA AGATHA CHARLES |
DIDAS Katona aliwahi kuwika takribani miaka mitano iliyopita, katika miaka hiyo alitumia zaidi vazi la kitenge kutengeneza mitindo mbalimbali ya nguo pamoja na viatu.
Hivi sasa amerejea kwenye tasnia hiyo akitumia ubunifu mpya, ikiwa ni pamoja na kuandaa onyesho la mavazi litakalotumia makopo ya bati kama moja ya vikorombwezo vya mavazi hayo.
Kurejea kwa Katona, safari hii kumemwezesha kuwa Meneja na Fundi Mkuu wa Kampuni ya Mavazi ya Katasawa ambayo iko chini ya Mkurugenzi wake, Sebastian Maganga.
Akizungumza na Jarida la ROSE wiki hii, Katona alisema anatarajia kufanya mapinduzi makubwa katika ulimwengu wa mitindo na hivyo ameandaa onyesho linalojulikana kama Septemba 15 Fashion Festival litakalofanyika Mikocheni katika Ukumbi wa Nafasi Art Space, hata hivyo tarehe rasmi la onyesho hilo bado haijapangwa.
Alisema katika onyesho hilo, atajikita zaidi kuonesha mavazi ya kipekee ikiwamo suruali yenye uwezo wa kuhisi pindi mtu anapokuibia mfukoni.
“Wategemee ubunifu mpya ikiwamo suruali inayoweza kuhisi kama mtu anakuibia na matumizi ya kopo ambalo lingetakiwa kutupwa mimi nitalitumia katika mitindo,” anasema Katona.
Katona aliwataja wabunifu watakaopanda jukwaani kumsindikiza kuwa ni pamoja na Ndesumbuka Merinyo (Mwafrika Merinyo), Kulwa Mkwandule, Asia Idarous na Taji Liundi.
Katona amewahi kuwavalisha wanamuziki katika video zao na mavazi ya kawaida kama Banana Zorro, Mrisho Mpoto, Peter Msechu na mwanamuziki raia wa Sweden SaRaha.