Na Jeremia Ernest, Mtanzania Digital
MISS Tanzania 2022, Halima Ahmad Kopwe ameshiriki uzinduzi wa kampeni ya Uzazi ni Maisha iliyoandaliwa na Shirika la AMREF Tanzania pamoja na Wizara ya Afya Zanzibar.
Ikumbukwe kuwa Mrembo huyo mbali ya kushinda taji la Miss Tanzania alinyakua taji dogo la mradi ambao ulilenga kuokoa vifo vya mama wajawazito wakati wa kujifungua.
Akizungumza na Mtanzania Digital amesema hii ni fursa kubwa kwake kwa sababu ni kampeni inayoendana na mradi wake ambao anatarjia kwenda nao shindano la Urembo la Dunia, hivyo amewasisitizia watu kuunga mkono kamapeni hiyo.
“Nimefurahi kuungana na kamapuni ya AMREF Tanzania na wizara ya afya Zanzibari katika kampeni hii ya Uzazi ni Maisha, niwaombe wadau kujitokeza kuungana nasi katika mbio zitakazo fanyika Agost 27, mwaka huu mahususi kwa ajili ya kuchangia vifaa tiba kwa uzazi salama,” amesema Halima Kopwe.
Naye Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo Mama Mariam Mwinyi ambaye ni mke wa Rais wa Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amesisitiza kuwa uboreshaji wa afya ya mama na mtoto ni jukumu la kila Mtanzania kwani taifa la kesho linategemena na afya ya mzazi wa leo.
Tukio hilo limehudhuriwa na wageni mbalimbali sambamba na Waziri wa afya Zanzibar, Nassor Mazrui na Mkurugenzi wa Clouds Media Group, Joseph Kusaga na Uongozi wa Shirika la AMREF Tanzania.